Ushahidi wa Anglo-Leasing kupeperushwa moja kwa moja kutoka Uingereza
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA inayosikiza kesi ya kashfa ya Anglo-Leasing itapokea ushahidi kwa njia ya mtandao kutoka Uingereza kuanzia Desemba 3 mwaka huu.
Hakimu mwandamizi Felix Kombo alifahamishwa na mwakilishi wa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kwamba mipango imefanywa kupokea ushahidi huo katika mahakama ya Milimani Nairobi kutoka mahakama ya Westminister, Uingereza.
“Mashahidi wawili watafika katika mahakama ya Westminister Uingereza na kupeperusha ushahidi wao moja kwa moja kuhusu kashfa ya Anglo-Leasing ambapo Serikali ilipoteza zaidi ya Sh43 bilioni,” Bw Kombo alifahamishwa.
Kiongozi wa mashtaka alisema sheria na utaratibu wa kuendeleza kesi za Uingereza ni “mashahidi wafike kortini na kutoa ushahidi kwa njia ya mtandao kisha wahojiwe na mawakili wa washtakiwa kutoka Kenya huku hakimu akinukuu ushahidi huo.”
Wakili Edward Oonge anayewakilisha washtakiwa Mabw Deepak Kamani, Rashmi Kamani , waliokuwa makatibu David Onyonka na Dave Mwangi alimweleza Bw Kombo ushahidi huo kutoka Uingereza utapeperushwa moja kwa moja na hautakuwa mgumu kufuata.
Washtakiwa hawa wamekana kushirikiana kuifilisi serikali mabilioni ya pesa katika mradi wa kuboresha maabara ya idara ya polisi na ununuzi wa mitambo ya kuweka mipakani kuwatambua wahalifu .
Kesi itaendelea Desemba 3, 2018.