Habari Mseto

Ushahidi wa Wako na Githu kuhusu Anglo-Leasing wasubiriwa

June 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa Mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Nicholas Mutuku Jumatano aliambia mahakama waliokuwa wanasheria wakuu Mabw Amos Wako na Prof Githu Muigai watafika kortini kutoa usahidi katika kesi ya ufisadi ya kashfa ya Anglo-leasing.

“Nilikuwa nimeorodhesha shahidi kutoka tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC kuingia kizimbani baada ya mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua lakini muda umeyoyoma sitaweza kumwita leo Jumatano,” alisema Bw Mutuku.

Bw Mutuku aliomba shahidi huyo akubaliwe atoe ushahidi wake mnamo Agosti kwa vile atajadilia masuala muhimu mno kuhusu kashfa hiyo.

Bw Mutuku alimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku kuwa mashahidi wengine walioorodheshwa kufika kortini Alhamisi ni waliokuwa wanasheria wakuu wastaafu Bw Amos Wako na Prof Githu Muigai.

Alimweleza hakimu kuwa mashahidi hao Mabw Wako na Muigai watawasili mahakamani Alhamisi  mwendo wa saa tatu unusu.

“ Nitaona ikiwa nitamwita afisa huyo wa EACC wakati mmoja na Mabw Wako na Muigai kwa vile sijui ushahidi wao utachukua muda gani,” alisema Bw Mutuku.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema wakati wa kusikizwa kwa kesi dhidi ya ndugu wawili Deepak Kamani , Rashmi Kamani na baba yao Chamnilal Kamani wanaoshtakiwa kwa kashfa ya Anglo-Leasing pamoja na waliokuwa makatibu wakuu David Onyonka , Dave Mwangii na Joseph Magari.

Washtakiwa walikanusha kuilaghai Serikali zaidi ya Sh3,8bilioni.