Utalii kudorora kufuatia mzozo kati ya Kenya na Tanzania
Na WINNIE ATIENO
WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wamemsihi Rais Uhuru Kenyatta angilie kati na kusuluhisha utata wa usafiri wa ndege kati ya Kenya na nchi jirani ya Tanzania.
Wawekezaji hao wanashtumu serikali ya Kenya kwa kuwalazimisha raia wa nchi jirani ya Tanzania kuwekwa karantini ya lazima kila wanapoingia nchini kufuatia janga la corona.
Kupitia muungano wa wadau wa utalii nchini yaani Shirikisho la Utalii la Kenya – Kenya Tourism Federation – wawekezaji hao walisema Kenya haifai kuwahukumu Watanzania kutokana na hatua yao ya namna wanavyokabiliana na janga la Covid-19.
“Tumewakosea wenzetu Watanzania na tunafaa kutafuta suluhu kwa sababu tukiendelea kuwatenga na kuwatema nje ya orodha ya raia wa nchi kadhaa ambao wanakubaliwa kuingia humu nchini Kenya bila vikwazo kama vile karantini, basi mzozo huu utaendelea na huenda hata wakafunga mipaka yao,” alisema mwenyekiti wa muungano huo Bw Mohammed Hersi.
Bw Hersi alionya kuwa huenda mzozo huo ukatokota zaidi baada ya Tanzania kupiga marufuku kampuni tatu za ndege za humu nchini.
“Hatua ya kuwatenga watanzania kwenye orodha ya raia wanaoruhusiwa nchini bila vikwazo ndio imetuletea balaa hii, hatuwezi kwenda kwa jirani zetu tunavyotaka ilhali hatutaki waje kwetu. Kainaya ni kwamba malori na mabasi yanapita mipakani bila vikwazo vyovyote,” aliongeza.
Bw Hersi alisema sekta za utalii, biashara na usafiri wa ndege zitabeba msalaba wa mzozo huo.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala kusisitiza kuwa raia wa nchi ambazo ziko katika hatari ya maambukizi ya corona ikiwemo Tanzania watawekwa karantini ya lazima wanapowasili humu nchini.
Bw Balala alisema raia hao watawekwa karantini ya lazima ya siku 14 kulingana na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri huyo alisema Kenya itaendelea kudumisha usalama wa watalii katika juhudi za kuimarisha sekta ya utalii.
Nchi hizo zimekuwa kwenye mzozo kuhusiana na swala la virusi vya corona huku Tanzania ikisisitiza imekabiliana na janga hilo.
Bw Balala alisema mipaka ya Kenya ingali imefungwa lakini watalii wanaoingia humu nchini kupitia viwanja vya kimataifa vya ndege ni sharti wafuate kanuni za afya ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
“Mipaka yetu ya barabara bado imefungwa lakini viwanja vyetu vya ndege viko wazi kwa watalii wa humu nchini na wale wa kimataifa kuzuru. Lakini tuna aina mbali mbali ya wageni; kuna wale wanaotoka nchi hatari zaidi, za maambukizi ya wastani na wale ambao wanatoka sehemu ambazo ziko shwari. Wale wanaotoka nchi ambazo zimetajwa hatari na WHO watawekwa karantini ya lazima kwa siku 14, ” alisisitiza Bw Balala ambaye alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wawekezaji wa sekta hiyo kupitia mawasiliano ya mtandaoni.?