Utata na ubovu wa ukumbi wa umma Eastleigh
Na MAGDALENE WANJA
KIKUNDI cha wanaharakati katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi kimemuandikia barua mkurugenzi wa mashtaka ya umma kikitaka kupelelezwa kwa jinsi shughuli za ukumbi mmoja wa umma – social hall – zinaendeshwa miaka 10 baada ya kandarasi yake kutolewa.
Kulingana na kikundi hicho cha wakazi, ukumbi huo ulio katika jengo la Eastleigh Social Hall uko katika hali mbovu na unakosa vitu muhimu kama vile maji, stima, na vyoo.
Ukumbi huo uko katika jengo la Eastleigh Social Hall ambalo lina biashara nyingi nyinginezo.
Kikundi hicho cha Eastleigh Residents Community Association pia kimeandikia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wakidai kuwa kandarasi kati ya serikali ya Kaunti ya Nairobi na kampuni inayomiliki jengo hilo haina uwazi.
“Licha ya kuwa na ofisi muhimu, ukumbi huo hauna stima wala vifaa vya kuwasaidia watu wenye ulemavu ambao wangetaka kufika katika ofisi hizo,” akasema Bw Osman Adow ambaye ni mkazi wa eneo hilo.
Paa la ukumbi huo halijakamilika huku sakafu yake ikiwe imebomoka.
Katika barua hiyo, wakazi hao wangetaka kandarasi hiyo kuwekwa wazi kwa wakazi ili kuwawezesha kujua haki zao na matarajio yao kutoka kwa kampuni iliyopewa kandarasi hiyo.
Wakazi hao pia wamelalamikia usalama wao wakidai kuwa kuta za jengo hilo si salama.