• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa KEBS wazua joto bungeni

Uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa KEBS wazua joto bungeni

 Na CHARLES WASONGA

WAZIRI msaidizi Biashara na Ustawi wa Kiviwanda Lawrence Karanja Jumanne alikabiliwa na wakati mgumu kutetea utaratibu uliotumiwa kumteua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa (KEBS) Benard Njiraini alipofika mbele ya wabunge.

Hii ni baada ya Mbunge wa Kipkelion Magharibi Hillary Kosgei aliyedai kuwa uteuzi wa Bw Njiraini haukufuata utaratibu wa kisheria. Alisema mkurugenzi huyo mkuu hakuwa bora zaidi kwani kuna wale waliopata alama za juu kumshinda katika mahojiano.

Bw Kosgei alisema katika shughuli ya uteuzi iliyoendeshwa mnamo Aprili 2019 na kampuni ya ushauri wa Delloite wale walioibuka bora walikuwa; Nixon Sigey aliyepata asilimia 82 za alama, Martin Chesire (asilimia 75) na Lucas Meso aliyepata asilimia 71.

“Lakini baada Baraza la Kitaifa Ubora (NCS) chini ya uenyekiti wa Kenneth Wathome kuwasilisha majina haya matatu kwa Waziri wa Biashara wakati huo alikataa majina hayo na kuamuru shughuli hiyo irejelewe tena. Haijulikani ni kwa nini Waziri alitoa uamuzi huo ilhali alipaswa kuteua mtu mmoja miongoni mwa watu hao watatu,” akasema mbunge huyo wa cha Jubilee.

Bw Kosgei aliongeza kuwa shughuli hiyo ya uteuzi iliporejelewa mnamo Agosti mwaka jana, orodha ya walioibuka bora katika mahojiano iliongezeka hadi kufikia watu watano.

Waziri Msaidizi wa Biashara na Viwanda Bw Lawrence Karanja akijibu maswali ya wabunge. Picha/ Charles Wasonga

Bw Geoffrey Murira alipata asilimia 76 ya alama, Nixon Sigey (asilimia 74), Martin Chesire (asilimia 72), Ishmael Shanje (asimilia 66) na Benard Njiraini aliyepata asilimia 64 ya alama zote.

Maelezo hayo yalikuwa kwenye stakabadhi ambazo Bw Kosgei aliwasilisha mbele wanachama wa kamati ya bunge kuhusu Biashara katika majengo bunge.

Waziri wa Kilimo Peter Munya ndiye alikuwa Waziri wa Biashara wakati ambapo uteuzi huo ulifanywa.

Lakini akijibu Bw Karanja alijikita kwenye mchakati wa uteuzi wa kwanza, aliosema kuwa uliendesha kulingana na taratibu za kisheria na ambapo Mkurugenzi Mkuu wa sasa (Bw Njiraini) aliibuka bora zaidi.

“Mheshimiw mwenyekiti ningependa kuihakikishia kamati hii kwamba uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu uliioendeshwa mnamo Agosti, 2019 kulingana na agizo la Waziri uliendeshwa kwa mujibu wa sheria husika,” akasema.

Hata hivyo wabunge; Geoffrey Oundo (Funyula), Nixon Korir (Lang’ata ) na Cornel Serem (Aldai ) walitilia shaka uhalali wa stakabadhi ambazo Bw Karanja aliwasilisha wakisema hazikuwa zimetiwa sahihi na Baraza la Kitaifa la Ubora (NSC).

Lakini Bw Karanja, ambaye alikuwa ameandanamana na Bw Njiarani (Mkurugenzi Mkuu wa KEBS) alisema hakufahamu kwamba wabunge walitaka atoe maelezo kuhusu utaratibu uliotumiwa katika uteuzi wa kwanza uliofanyika Aprili, 2019

“Ni wazi kuwa utaratibu wa kisheria haukuzingatiwa wakati wa uteuzi wa Bw Njiraini. Ni wazi kuwa mkurugenzi huyu aliyeteuliwa aliibuka nambari sita bora miongoni mwa walioorodheshwa na watu wengine bora walipitwa na ndipo akateuliwa,” akasema Dkt Oundo.

Kwa sababu wabunge hawakuridhisha na maelezo na Waziri Msaidizi Bw Karanja, mwenyekiti wa kamati hiyo Kanini Kega aliamuru kwamba Waziri wa Biashara Betty Maina afike mbele ya kamati hiyo Jumanne juma lijalo ili atoe maelezo zaidi kuhusu suala hilo.

You can share this post!

Wiyeta na Laiser Hill mabingwa wa Chapa Dimba Bonde la Ufa

Trump atakataa kutengwa licha ya kutangamana na wanaougua...

adminleo