• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Utovu wa usalama Matungu wazidi mtoto wa miaka 7 akiuawa

Utovu wa usalama Matungu wazidi mtoto wa miaka 7 akiuawa

Na PETER MBURU

HALI ya utovu wa usalama katika eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega imezidi kutokota licha ya wakuu wa usalama kuzuru eneo hilo na baadhi ya viongozi kukamatwa.

Hii ni kufuatia kisa ambapo mtoto wa miaka saba aliuawa kwa kudungwa kisu Jumapili, wakati wakora walipovamia nyumbani kwao.

Mvulana huyo ambaye alikuwa darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Star Academy aliripotiwa kudungwa mara kadhaa mgongoni, hadi akafa.

Polisi wanachunguza kisa hicho ambacho kilitokea siku chache tu baada ya seneta wa kaunti hiyo Cleophas Malala, mbunge wa Matungu Justus Murunga, diwani wa Mayoni Libinus Oduor na aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa kukamatwa kuhusiana na visa vya watu kuuawa.

Vilevile, mauaji ya mtoto huyo yalitokea Jumapili, siku ambayo wanasiasa hao waliachiliwa na polisi.

Mavamizi ya watu eneo hilo yamesababisha mauaji ya watu 20 katika kipindi cha miezi miwili, huku 50 wengine wakiachwa na majeraha mabaya. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Mayoni, Lubanga, Mung’ungu, Munami, Ejinja, Ogalo, Lung’anyiro, Harambe, Sayangwe na Koyonzo.

Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i wiki iliyopita alizuru eneo hilo na kusema aparesheni kali ya polisi ingeanzishwa, kukabili wavamizi hao.

You can share this post!

Umaskini na ardhi kiini cha uhalifu Kiambu

Gavana motoni kwa kuficha nakala za kuonyesha alivyotumia...

adminleo