VALENTINO: Wakazi wa Nakuru walivyojitolea kutoa damu
NA RICHARD MAOSI
WAKAZI wa Nakuru Alhamisi walimiminika mjini humo kusherehekea Valentino Dei kwa ukarimu na furaha ya aina yake.
Barabara ya Kenyatta, na ile ya Moi ilifurika vijana kwa wazee na kunogesha biashara ya kuuza na kununua maua kwa wapenzi huku kila mmoja akipania kukonga moyo wa muhibu wake kwa mahaba motomoto.
Taifa Leo Dijitali ilikita kambi katika eneo la uwanja wa Standard Chartered mkabala wa soko la Maasai eneo maarufu kwa biashara ya mikufu na shanga.
Shughuli ya kutoa damu hufanyika kila mwaka hapa siku hii, ikiongozwa na Kenya National Blood Transfusion Service (KNBTS), shirika la St John Ambulance na Msalaba Mwekundu.
Kulingana na katibu wa uhusiano mwema wa KNBTS Bw Joseph Kamotho, Kenya ina uhaba wa damu takriban mifuko 5000.
“Ukitaka kuonyesha mtu kuwa unampenda na kumjali bila shaka kuna mbinu mbalimbali za kuwasilisha ujumbe, na siku kama hii ni mojawapo ya njia kutoa taswira mwafaka,” alisema.
Wakazi wa Nakuru kutoka kila kabila rangi na jamii, bila kujali umri walijitolea kuonyesha kuwa wanajali maslahi ya wale wanaohitaji damu ya dharura.
Harrison Mwangi mwanafunzi kutoka katika Chuo Kikuu cha Cha St Paul anasema ni wajibu wake kutoka moyoni kutoa damu kila mwaka bila kusukumwa na mtu.
Yeye hufanya hivi kutokana na haja ya uhitaji mkuwa wa damu miongoni mwa Wakenya wengi wanaotaabika hospitalini.
Hii ikiwa na mara yake ya tatu, alieleza ni fahari kubwa kufanya jambo hili hususan katika swala la kuokoa maisha ya binadamu wenzake.
“Siku ya Valentino mbali na kusherehekea na wale tunaowapenda, ni muhimu pia kujihusisha katika zoezi la kurudisha mkono katika jamii kwa vitendo,” alisema.
Kwingineko Juliet Nabwire mwanafunzi katika taasisi ya KMTC, anasema hushiriki katika zoezi la kutoa damu kila mwaka ili kuwaokoa manusura wa ajali.
Anaamini kaunti ya Nakuru imekuwa ikishuhudia ajali nyingi hasa barabara ya Salgaa na Sachangwan kila mwaka,na hali hii imekuwa desturi.
“Nilikuwa nimekuja katika benki nikiandamana na mzazi wangu ili kulipa karo ya shule nilipokuta shughuli hii muhimu ikiendelea na bila shaka singeondoka bila kutoa damu,”alisema.
Huduma ya msalaba mwekundu imeomba wakenyakutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kujaza nakisi ya damu inayoshuhudiwa nchini.
Zoezi hili linapania kuwaokoa wagonjwa mahututi na akina mama wajawazito wanaohitaji damu ya dharura katika hospitali za serikali na za kibinafsi kote nchini.
Mwanachama wa kujitolea katika shirika la msalaba mwekundu Prudence Kiprocho,aliwaomba wakenya kujitolea katika zoezi la kutoa damu akisema ni kwa manufaa ya wapendwa wao.
Aidha waliotoa damu walipokezwa maua mekundu ya waridi kwa kuonyesha mapenzi ya dhati na utu kupitia ishara ya kujali maslahi.
Kwa Upande mwingine biashara ya kuchuuza maua karibu na eneo la kutoa damu ilinoga.
Everlyn Mogaka mwanafunzi wa uzamili kutoka Chuo cha Kenyatta,jijini Nairobi anasema amekuwa akifanya kazi ya kuuza maua kila mwaka.
Alijipatia ujuzi wa kutengeneza miundo tofauti ya kupendeza kabla ya kuifikisha sokoni Februari 14 kila mwaka.
Anasema kipato cha kuchuuza maua ni kizuri, kwani ni njia mojawapo ya kujipatia kipato cha ziada bali na kutangamana na watu mbalimbali wenye hisia za mapenzi.
“Biashaya yenyewe japo ni ya siku moja tu kila mwaka inaweza kunitengenezea hela nzuri kwa muda mfupi,” alisema.
Tangu sherehe za Valentino Dei zianze kusherehekewa miaka 200 iliyopita, wapenzi wamekuwa wakizitumia kununuliana zawadi kudhihirisha mapenzi yao.