• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 2:30 PM
Viboko wanavyohangaisha wakazi Matayos

Viboko wanavyohangaisha wakazi Matayos

GAITANO PESSA

WAKAZI wa kijiji cha Buroboi katika wadi ya Matayos Kaskazini, eneobunge la Matayos wanazidi kukadiria hasara baada ya viboko kuvamia mashamba yao na kuharibu mimea.

Wakiongozwa na Leonard Wandera, wakulima hao wadogo wenye gadhabu wamesema viboko hao wanaoishi katika mto Sio wamekuwa wakivamia mashamba yao nyakati za usiku wakitafuta chakula msimu huu wa kiangazi.

Uharibifu umeshudiwa katika mashamba yenye mboga, viazi vitamu na mabingobingo (napier grass).

“Tumekadiria hasara kutokana na uharibifu wa vyakula vyetu. Tunaishi kwa hofu ya kushambuliwa na Wanyama hawa hasa alfajiri na usiku. Viboko hawa pia ni tishio kwa wanafunzi wanaoelekea shuleni asubuhi,” amesema Wandera

Mary Akinyi, mkazi mwingine, ameitaka shirika la huduma kwa wanyama pori, KWS kuingilia kati na kuhamisha viboko hao ili kuzuia uharibifu zaidi.

“Viboko wameguza mashamba yetu kuwa malisho. Tuliwafahamisha maafisa wa KWS ambao waliwafukuza Wanyama hao hadi mtoni lakini wao hurejea usiku. Tunataka waondolewa kabisa,” amesema Akinyi.

Wanakijiji sasa wameitaka KWS kuwafidia la sivyo wachukue sheria mikononi kwa kuwawinda viboko hao, kuwauwa na kuwafanya kitoweo.

Diwani wa eneo hilo Linus Asiba aliyewaunga mkono wakazi ameitaka KWS kuchukua hatua za haraka ili kuwaondolea wakazi hasara na wasiwasi.

“Mwaka jana tulikumbana na masaibu sawia. KWS inapaswa kujukumika vilivyo kutatua mzozo kati ya Wanyama na wanadamu kwa sababu nahofia kuwa iwapo watachukulia sheria mikononi mwao ni viboko watakoumia,” amesema na kuongeza kuwa chui pia wamekuwa wakiwahangaisha wakazi.

You can share this post!

Mwanamume taabani kwa kujifanya mkewe Ruto

Unyama wa kutisha mwanamke mgonjwa kuuawa

adminleo