• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Kiboko ahangaisha wakazi wa kijiji cha Nyachaba

Kiboko ahangaisha wakazi wa kijiji cha Nyachaba

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Nyachaba, Juja, Kaunti ya Kiambu, wamejawa na hofu kwa sababu kiboko anawahangaisha.

Bw David Kariuki, mkazi wa kijiji hicho anasema wameshindwa kwenda kufanya kazi shambani na hata kuchota maji ya mto Ndarugu kwa sababu ya kiboko huyo.

Alisema kiboko huyo ameharibu mimea katika kijiji hicho na hali ni mbaya kiasi kwamba wakazi hao wanaiomba serikali kuingilia kati ili kuwasaidia.

Hasa wanataka Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) lifanye haraka ili kumuondoa mnyama huyo.

Alisema kwamba Jumatano wiki jana kiboko huyo aliwavamia wanawake wawili walipokuwa wakienda shambani.

Mzee wa Kijiji Bw Francis Gitau alisema wanahofia usalama wa watoto wao ambao hurauka kuenda shuleni majira ya asubuhi.

“Kiboko huyo huonekana asubuhi na mapema na majira ya jioni. Kwa hivyo kuwepo kwake katika eneo hili ni hatari kwa usalama,” akasema Bw Gitau.

Aliiomba serikali kupitia KWS kuingilia kati kuona ya kwamba kiboko huyo anatolewa ili apelekwe mbali na binadamu kuzuia mgogoro.

Naye Bi Martha Mugure wa kijiji hicho anasema kuwa wakazi wamejawa na hofu huku wakishindwa la kufanya.

Alisema wanakijiji wameamua kutembea kwa vikundi kwa sababu wanahofia kushambuliwa wakati wowote.

Naye mwanafunzi Faith Wanja alisema wanafunzi wengi hawarauki mapema kwenda shuleni kwa sababu ya kuogopa kupatana na kiboko huyo.

Alisema wazazi wengi wameamua kuwasindikiza wana wao shuleni wakihofia mnyama huyo anaweza akasababisha madhara mabaya.

Wakazi wengi katika eneo hilo wanaishi karibu na mto ambapo wanaendesha kilimo cha mboga, nyanya na viazi.

You can share this post!

WANGARI: Mikakati yahitajika kupunguza mzigo wa matibabu...

Viongozi wamwomboleza wakili Evans Monari