Habari Mseto

Vihiga kusajili wakulima 2,500 kukuza mboga za kienyeji

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA DERICK LUVEGA

SERIKALI ya Kaunti ya Vihiga imeanza kuwasajili wakulima 2,500 watakaoshiriki katika mradi wa ukuzaji wa mboga za kienyeji utakaofadhiliwa kwa kima cha Sh30 milioni.

Mradi huo unaoendeshwa na idara ya biashara na kilimo ya kaunti pia utahakikisha wakulima hao wanapata mbegu kuanzia wiki ijayo kwa matayarisho ya msimu wa upanzi.

Mbegu hizo zitatolewa na kiwanda cha bidhaa za kiasili (NPI) na chuo kikuu cha Jomo Kenyatta na zitakuwa za mboga za kienyeji maarufu katika eneo hilo kama tsisaga, tsimboga, likuvi na mutere.

Waziri wa biashara wa kaunti Geoffrey Vukaya alisema mradi huo uliasisiwa baada ya kongamano la kibiashara lililoandaliwa Vihiga katikati ya mwaka huu na unalenga kubadilisha kaunti hiyo kuwa kituo kikuu cha kibiashara kwa mauzo ya mboga za kiasili.

“Ingawa mashamba yetu ni madogo madogo, uzalishaji mboga za kienyeji utawasaidia sana wakulima wetu. Tuliamua kuanza na wakulima 2,500 kisha baadaye tutaongeza idadi hiyo,” akasema Bw Vukaya.

Vile vile, kaunti ya Vihiga imetambua Supamaketi ya Carrefour jijini Nairobi kama moja ya masoko ya mboga hizo za wakulima.

“Supamaketi ya Carrefour imekubali kununua mboga za kienyeji moja kwa moja kutoka kwa wakulima ili kuziuza kwa wateja wao. Pia tutaweka vituo vya kuzikusanya katika maeneo ya Walodeya mjini Chavakali, Wemilabi kule Emuhaya, mjini Majengo na Cheptulu inayopatikana Hamisi,” akasema Bw Vukaya.

Chuo kikuu cha JKUAT pia kitawapa wakulima hao mafunzo ya kilimo cha vyakula vya kiasili baada ya chuo hicho kutia saini mkataba wa makubaliano na serikali ya kaunti mnamo Juni, mwaka huu.