Vijana sasa wajipata mateka wa mikopo ya simu
Na MWANDISHI WETU
MAELFU ya vijana jijini Nairobi sasa ni mateka wa madeni baada yao kushindwa kulipa mikopo wanayochukua kupitia simu zao.
Vijana hao sasa wamesajiliwa katika shirika linalohifadhi takwimu za watu wanaoshindwa kulipa mikopo (CRB). Kwa kawaida watu wanaoorodheshwa katika shirika la CRB hawaruhusiwi kuchukua mikopo zaidi.
Wengi wa vijana huchukua mikopo kupitia programu za simu (apu) ili kupata fedha za kushiriki michezo ya kamari kama vile kutabiri matokeo ya mechi.
Mikopo ya simu hupatikana kwa urahisi lakini hutozwa kiasi kikubwa cha riba. Mikopo hiyo hutolewa na benki au tasisi nyinginezo zisizo benki.
Idadi kubwa ya vijana huchukua mikopo hiyo bila kufahamu kanuni na masharti yake hivyo kujipata pabaya wanaposhindwa kulipa.
Mkurugenzi Mkuu wa TransUnion CRB Billy Owino anasema kuwa kuna haja ya vijana kupewa mafunzo kuhusiana na matumizi ya fedha ili kuwaepusha kujiingiza katika madeni ambayo huwalemea baadaye.
“Shirika la CRB, halitafuti watu wanaoshindwa kulipa mikopo yao. Sisi hupokea majina kutoka kwa taasisi za kutoa mikopo ya kifedha kila mwezi,” akasema Bw Owino.
“Taasisi za kifedha zinapowasilisha majina ya walioshindwa kulipa mikopo, tunakagua taarifa hizo ili kubaini ikiwa kuna dosari. Majina yaliyo na taarifa sahihi yanahifadhiwa na kupewa kwa taasisi mbali zinazotaka kufahamu uadilifu wa waombaji wa mikopo,” akaongezea.
Shirika la CRB huwapa alama watu walioshindwa kulipa mikopo kuanzia AA, BB, C, D, E, F na J. Watu waliopewa alama ya J huwa katika hatari kubwa ya kunyimwa mikopo na karibu taasisi zote za kifedha.
Wateja wanaotaka majina yao kutolewa katika orodha ya CRB hutakiwa kulipa madeni na kisha kulipa ada ya ShSh2,200 ili kupewa cheti cha kuondolewa rasmi.
Historia ya mkopaji, hata hivyo, husalia ndani ya faili za CRB kwa muda wa miaka mitano licha ya mteja kupewa cheti cha kuondolewa lawama.
Kwa kawaida taasisi ya kifedha hupeleka majina ya wateja wake kwa CRB baada ya kukataa kulipa mkopo kwa kipindi fulani.
“Wateja wanaotaka kupata taarifa ikiwa wameorodheshwa katika CRB wanaweza kutumia nambari 21272. Kadhalika tuko na programu ya ‘Nipashe App’ ambayo wateja wanaweza kutumia kupokea taarifa,” akasema Bw Owino.