Habari Mseto

Vijana wanavyoponzwa na ulevi na ukahaba

June 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

VIJANA waliokuwa wameandaliwa kikao cha kutafuta mbinu za kufanya Mji wa Murang’a uafikie biashara ya masaa 24 wamesema kinachohitajika ni kukubaliwa kwa makahaba warembo wahudumu katika mitaa ya eneo hilo.

Kikao hicho katika ukumbi wa Manispaa ya Murang’a kiliandaliwa Jumamosi chini ya ufadhili wa serikali ya Kaunti pamoja na wawekezaji wa kibinafsi.

Ni kikao ambacho kilibakia kimeduwazwa na ujasiri wa vijana hao na pia kuzua mjadala mkali kuhusu msukumo wa kimaisha wa wengi wao.

Walishikilia kuwa biashara inayoweza ikafanikiwa ni ile ya uuzaji vileo na kisha kuwe na warembo mitaani.

Bw Eliud Kirika wa miaka 24 alipoamka kutoa mchango wake kwa niaba ya vijana alisema kuwa kwa sasa mji huo uko na makahaba wasio wa kupendeza macho hivyo basi kuwafanya wanaume wasusie mji huo.

“Pia, hatua ya serikali ya kuweka vikwazo uuzaji wa pombe kwa masaa 24 imewafanya wanaume wasiwe na la kufurahia katika mji huu. Kishawishi cha mwanamume kutumia pesa ni raha na wakati umeweka vikwazo katika raha, basi unafukuza wanaume mjini,” akasema.

Hatua ya mshirikishi wa mkutano huo, Bw James Njoroge ya kumtaka kijana huyo aketi kwa msingi kuwa mchango wake ulikuwa wa ucheshi ulikumbana na kelele za pingamizi kutoka kwa vijana waliokuwa katika ukumbi huo wa Murang’a.

“Anasema ukweli! Huo ndio mchango wetu wa kuafikiana na hakuna mahali amepotoka. Hivyo ndivyo tumekubaliana achangie nka ukimuamrisha akae chini hata sisi tutatoka nje,” akateta mmoja wa vijana huyo akijifahamisha kama Titus Njogu.

Bw Kirika aliendelea mbele na mchango wake akisema kuwa kwa sasa mji wa Murang’a uko na makahaba 16 pekee na ambao wamezoeana na wanaume kiasi kwamba kunahitajika wengine wakubaliwe kufanya biashara yao mjini bila vikwazo.

“Hawa makahaba 16 huwa wanawafukuza makahaba wapya. Hawataki ushindani kamwe. Lakini ukiwatazama, ni wale tu wamekuwa mjini humu kwa zaidi ya miaka 15 hivyo basi kuishiwa na ule uvutio kwa wanaume.

“Sura zao ni tosha kuwafanya wanaume walio na hela za kutumia waelekee katika miji mingine kusaka raha,” akasema.

Aliteta kuwa mji ambao haukubalii makahaba wawe na Uhuru wao na wawe tu ni wale warembo, kisha mji huo ukose kukubalia uuzaji wa pombe bila vikwazo na mtaani kukubaliwe uuzaji wa miraa, basin i sawa na kuua uchumi wa eneo hilo.

“Mimi naongea ukweli ulio uchi kabisa. Biashara ya usiku wa manane huwezi ukatarajia watu wakuje kununua unga au mavazi. Masaa ya usiku ni ya wasakao raha. Kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tatu usiku, unaweza ukapigia debe biashara zile za kawaida. Lakini kuanzia saa nne usiku hadi asubuhi ya saa 12, biashara ni ulevi na mahaba,” akasema Kirika akishangiliwa na wenzake.

Alisema kuwa biashara za usiku hazitakuwa zikizingatia sana wanawake kwa kuwa kwa kawaida wao sio wa kuhatarisha maisha yao kwa giza ya usiku mjini.

Alipendekeza kuwa maafisa wa polisi wazimwe kuhangaisha wanaosaka raha usiku mjini humo, akitaka wawe tu wakisaka wezi pekee.

“Mji wetu unaishiwa na pesa usiku kwa kuwa wale wote wanaosaka raha zao masaa hayo huwa wanakumbana na hatari ya kukamatwa na maafisa wa polisi. Unashindwa kuelewa ni kwa nini mtu ambaye ameamua kutumia pesa zake usiku anahangaishwa huku wezi wakiwa tele kwa giza,” akasema.

Mwakilishi wa afisi ya gavana katika mkutano huo, James Gathuita alitaja kauli hizo kuwa za kipekee na ambazo zinaangazia hali halisi ya fikira za vijana wa taifa hili.

“Sitaki kuwalaumu au kuwaunga mkono kwa kuwa dunia iko hivyo. Lakini ni ishara tosha kuwa tuko na shida kubwa ya kimtazamo miongoni mwa vijana wetu,” akasema.