Habari MsetoSiasa

Vilio katika kaunti baada ya mishahara kucheleweshwa

February 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa kaunti kadhaa wanateseka kwa kukosa mishahara tangu Desemba, huku wananchi wakikosa huduma muhimu kutokana na uhaba wa fedha.

Mwaka uliopita, Serikali Kuu ilisema haitatuma fedha kwa kaunti zinazodaiwa na wafanyabiashara hadi zimalize kulipa madeni.

Kaunti 28 ziliathirika na agizo hilo lililolenga kukomesha mtindo wa magavana wapya kukataa kulipia huduma zilizotolewa kwa kaunti zao wakati wa utawala uliotangulia.

Baadhi ya magavana wamekuwa wakijitetea kwamba hawaezi kulipia huduma au bidhaa ambazo zilitolewa kwa njia zilizokiuka sheria kwani watalaumiwa ikibainika kulikuwa na ufisadi.

Katika Kaunti ya Nandi, wafanyakazi wa bunge la kaunti hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu sasa. Spika wa bunge la kaunti hiyo, Bw Joshua Kiptoo alisema zaidi ya wafanyakazi 4,000 wanateseka kwani hawajalipwa tangu Novemba.

“Wengine wamefukuzwa katika nyumba walizokodisha na kuna baadhi ambao watoto wao wamefukuzwa shuleni kwani hawajalipiwa karo,” Katibu wa Chama cha Watumishi wa Umma, tawi la Nandi, Bw John Agaga akasema.

Katika Kaunti ya Kisii, zaidi ya wafanyakazi 6,000 waliambiwa mshahara wao wa Januari ungechelewa kwa kuwa Wizara ya Fedha ilichelewa kutuma pesa kwa kaunti hiyo.

Hali sawa na hii ilishuhudiwa katika Kaunti ya Trans Nzoia ambapo sasa wauguzi wametishia kususia kazi kwani hawajalipwa mishahara tangu Desemba.

Walisema suala la serikali kuu kuchelewesha pesa halifai kuwa sababu ya wao kutolipwa mishahara kwani wafanyakazi wa vyeo vya juu wanapokea malipo yao.

“Baadhi ya maafisa wakuu wanazidi kunenepa huku wanachama wangu wakikonda kwa ajili ya mahangaiko. Ni ukatili kwa maafisa hao kuendelea kushiba ilhali sisi tuna njaa,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN), tawi la Trans Nzoia, Bw Willy Sifuna.

Wafanyakazi katika idara ya afya ya Meru pia walitishia kuanza mgomo wakisema serikali ya kaunti hiyo haijawasilisha ada mbalimbali zinazogharimu Sh38 milioni za Novemba na Desemba.

Ada hizo ni pamoja na mikopo ambayo wafanyakazi walichukua katika benki, hali inayotishia mali zao kupigwa mnada.

“Tetesi kwamba serikali ya kaunti itashauriana na mabenki kuhusu kuchelewa kulipa madeni halina msingi. Wanachama wetu wametuagiza tuitishe mgomo haraka iwezekanavyo,” akasema Mwenyekiti wa KNUN, tawi la Meru, Bw Bakari Munoru.

Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alisema kaunti ambazo zilikamilisha madeni yao niBaringo, Elegeyo Marakwet, Embu, Homabay, Kajiado, Kericho, Kilifi, Kitui, Kwale, Laikipia, Makueni and Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Uasin Gishu na Lamu.

Kaunti nyingine tisa ambazo ni Nakuru, Taita Taveta, Tana River, Trans Nzoia, Machakos, Bungoma, Kakamega, Murang’a na Kisii zimepiga hatua vyema kulipa madeni.

Alisema Nandi, Marsabit, Kiambu, Meru, Kisumu, Tharaka-Nithi, Mombasa na Busia zimetoa mapendekezo kuhusu jinsi zitakamilisha madeni hayo kufikia Juni.

Kwa upande mwingine, kaunti za Turkana, Garissa, Wajir, Narok, Nairobi, West Pokot, Siaya, Kirinyaga, Bomet, Isiolo, Mandera, Samburu, Migori na Vihiga hazijapiga hatua.

Ripoti za Tom Matokeo, Sharon Achieng, Gerald Bwisa, David Muchui na Francis Mureithi