Viongozi Magharibi wamtaka Rais atimize ahadi ya kufufua sekta ya sukari
SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA
WABUNGE wa Jubilee kutoka Magharibi mwa Kenya wameitaka serikali kufadhili mpango wa ustawishaji kilimo cha miwa kufufua sekta hiyo inayokabiliwa na changamoto nyingi.
Wabunge hao; Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Didmus Barasa (Kimilili) na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale Jumatano waliitaka serikali kuwekeza fedha katika shughuli ya utafiti wa miwa ili kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.
“Ili kufufua sekta ya sukari, serikali ianze kufadhili shughuli kama utafiti ili kuwezesha viwanda vya humu nchini kupata malighafi tosha. Hii hatua ya kufutilia mbali mzigo wa madeni kwa viwanda vinavyomilikiwa na serikali haitasaidia zaidi ikiwa kiwango cha uzalishaji miwa nchini kitasalia chini,” akasema Dkt Khalwale.
Naye Bw Washiali akasema: “Ili kufufua sekta ya sukari, tunataka kuona trekta zikilima mashamba kwa ajili ya uzalishaji miwa. Tunataka kuona serikali ikifadhili utafiti kando na kukarabati mashine kuukuu katika viwanda vya miwa.”
Viongozi hao hata hivyo walimsuta Rais Uhuru Kenyatta kwa kufeli kutimiza ahadi alizotoa kwa wakulima wa miwa Magharibi mwa Kenya.
“Baada ya kufeli kutimiza ahadi alizotoa kwa wakulima kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 sasa ameamua kuwatumia magavana na Waziri Eugene Wamalwa kuendeleza kampeni ya ufufuzi wa sekta ya viwanda katika eneo hilo,” akasema Bw Washiali kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu.
“Kile tunataka kuona ni suluhu la kudumu kwa changamoto inayowakabili wakulima wa miwa wala sio ahadi za kisiasa,” akasema mbunge huyo ambaye Juni 2020 alipokonywa wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.
Viongozi hao walipuuzilia mbali hatua ya Waziri wa Kilimo Peter Munya ya kupiga marufuku uagizaji sukari wakisema ni njama ya kutoa nafasi ya kuuzwa kwa sukari ambayo iliagizwa kupita kiasi mwaka 2019.