Viongozi wa kidini waombea Waiguru na madiwani wapatane
Na GEORGE MUNENE
VIONGOZI wa kidini sasa wameamua kuombea Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na madiwani wa kaunti hiyo ili wamalize mzozo unaotisha kulemaza huduma katika kaunti hiyo.
Wakati wa maombi waliyofanya mjini Kutus na kushirikisha madhehebu mbalimbali, viongozi wa kidini walisema kuwa wananchi ndio wanaathiriwa na vita hivyo.
Walitoa wito kwa wanasiasa hao kupatana kwa ajili ya amani na maendeleo katika kaunti hiyo.Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Kianglikana dayosisi ya Kirinyaga, Joseph Kibucwa, viongozi hao walielezea hofu kwamba vuta nikuvute hiyo inaathiri utendakazi wa serikali ya kaunti.
Wabunge wote wa kaunti hiyo hawakuhudhuria shughuli hiyo isipokuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Wangui Ngirici na madiwani watatu kati ya jumla ya 33.
Gavana Waiguru pia hakufika katika mkutano huo wa maridhiano japo aliwakilishwa na waziri wa ardhi katika Kaunti ya Kirinyaga, Kasisi Samuel Kanjobe.
Hata hivyo, mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Jubilee tawi la kaunti ya Kirinyaga Mureithi Kang’ara ambaye alisifu maombi hayo.
Viongozi hao walikariri umuhimu wa kuwepo kwa umoja miongoni mwa viongozi waliochaguliwa ili kuwe na mazingira bora ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wakazi.
Walisema wanasikitika kuwa viongozi wanalumbana huku wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma katika takriban idara zote za serikali hiyo.
“Viongozi wakipigana na wananchi huumia,” akasema Askofu Kibucwa.Waliwataka Gavana Waiguru na Madiwani hao kusameheana na kukomesha malumbano ili amani irejee katika kaunti ya Kirinyaga.
Viongozi hao wa kidini walielezea hofu ya kaunti hiyo kushindwa kuweka mikakati ya kudhibiti janga la Covid-19 ikiwa gavana huyo na madiwani wataendelea kuzozana.