Viongozi wa kidini washinikiza Handisheki ya Ruto na Gachagua
BARAZA la Maimamu na Wahubiri nchini (CIPK) limewataka Rais William Ruto na wake Rigathi Gachagua kuzika tofauti zao za kisiasa, kwa minajili ya maendeleo nchini.
Mwenyekiti wa CIPK North Rift Sheikh Abubakar Bini pamoja na Imam wa msikiti wa Masjid Noor, Awadhi Jamal walisema viongozi hao wanapaswa kuungana na kuendelea kufanya kazi pamoja badala ya kuanika tofauti zao mbele ya umma.
Wakizungumza Jumatatu, Juni 17, 2024 katika msikiti wa Masjid Noor mjini Eldoret wakati wa kusherehekea siku ya pili ya Idd-Ul-Adha, viongozi hao walielezea hofu kwamba mabishano kati ya viongozi hao wawili yana uwezekano wa kuzidisha uhasama miongoni mwa wafuasi wao.
“Inasikitisha kwamba rais wetu na naibu wake ni wanachama wa UDA chini ya muungano wa Kenya Kwanza lakini wanaanika tofauti zao hadharani jambo ambalo ni hatari kwa umoja wa nchi yetu,” alisema Sheikh Bini.
Sheikh Bini alisikitika kwamba uhasama huo sio tu wa kuchochea uhasama miongoni mwa wafuasi wao, bali pia utaathiri maamuzi muhimu serikalini akitoa mfano wa mjadala unaoendelea kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024.
Sheikh Bini alisema kutoelewana kati ya Rais Ruto na Bw Gachagua kutaathiri pakubwa mwananchi wa kawaida.
“Tofauti kati ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua inatia hofu hasa wakati ambapo bunge linatarajiwa kujadili Mswada wa Fedha wa 2024 ambao una athari kubwa kwa Wanjiku. Tunachowaambia viongozi hao wawili ni kuweka kando tofauti zao na kuhakiki mswada huo ili kufuta masuala yanayopingwa na Wakenya kwenye mapendekezo yake kwa kufanya kazi pamoja kama viongozi wanaothamini kilio cha Wakenya waliowachagua ili kufaidika na sheria zilizopitishwa na mabunge yetu,” akasema Sheikh Bini.
Imam Awadhi aliunga mkono kauli ya Sheikh Bini, akimtaka Rais Ruto kuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha umoja wa Wakenya wote akikumbuka kuwa rais ni ishara ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, alitoa wito kwa jamii ya Waislamu kuunga mkono uongozi wa Rais Ruto kwa kuombea nchi na kuepusha tofauti ambazo zinaweza kuzua mifarakano nchini.
Hata hivyo, alitoa wito kwa Waislamu kuunga mkono uongozi wa Dkt Ruto kwa kuombea nchi na viongozi wote kwa jumla.
Aidha amewataka Waislamu kuzika tofauti katika kusherehekea Idd-ul-Adha.
“Jukumu letu sisi viongozi wa Kiislamu ni kuwaombea dua viongozi wote na tofauti katika sherehe zisilete mifarakano. Ombi letu ni kwamba Wakenya kupitia uongozi wa Rais William Ruto na naibu wake waendelee kufanya kazi pamoja ili kuvutia baraka za Mungu,” alisema Imam Awadhi.
Katika siku za hivi karibuni, Rais Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua wameonekana kukosoana hadharani hasa kupitia wandani wake.
Pendekezo la Bw Gachagua kuhusu mfumo wa ugavi wa raslimali; mtu mmoja, kura moja, shilingi moja, limeonesha tofauti kati ya viongozi hao wa hadhi ya juu nchini.
Dkt Ruto na Bw Gachagua, walichaguliwa Agosti 2022 kama Rais na Naibu Rais, mtawalia.