• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Viongozi wamsifu Rais Kenyatta kuteua Munya Waziri wa Kilimo

Viongozi wamsifu Rais Kenyatta kuteua Munya Waziri wa Kilimo

Na Charles Wanyoro

BAADHI ya viongozi wa Kaunti ya Meru wamekaribisha kupandishwa cheo kwa Waziri mpya wa Kilimo Peter Munya, wakisema atasaidia kufufua sekta ya kilimo.

Wabunge Rahim Dawood(Imenti Kaskazini), Paul Mwirigi(Igembe Kusini) na Mpuru Aburi(EALA) walisema uteuzi huo uliofanywa na Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumanne, ni afueni kwa wakulima wote nchini.

Wakizungumza maeneo tofauti, wabunge hao walisema walikuwa na uhakika kwamba Bw Munya atayashughulikia matatizo yanayozonga sekta ya kahawa, chai, maziwa na miraa kwa sababu anaelewa masaibu yao.

Bw Aburi alisema kwamba aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri hakuwa na uwezo wa kuchapa kazi jinsi ilivyotarajiwa huku akimlaumu kwa kusababishia wakulima wa miraa mahangaiko makubwa.

“Naunga mkono uteuzi wa Bw Munya kwa sababu anaelewa shida mbalimbali ambazo zinakumba eneo hili. Yeye ni mchapakazi na ana roho ya uwajibikaji. Nilikuwa nimelalamika kwamba Bw Kiunjuri alikuwa amelala kazini na sasa nina furaha Rais amesikia kilio chetu,” akasema.

Mabw Dawood na Mwirigi wakati huo walitoa wito kwa Bw Munya aanze kazi mara moja kwa kutoa mwelekeo kuhusu unyunyiziaji wa kemikali katika maeneo yaliyovamiwa na nzige hao.

“Nina hakika kwamba atawajibika na kuwamaliza nzige hao ili kuhakikisha hakuna njaa. Anatoka eneo ambalo kilimo kimeshamiri na tuna imani kwamba atahakikisha kahawa, majani chai na miraa inauzwa kwa bei nzuri,” akasema Bw Dawood.

Bw Mwrigi pia alimsifu Rais kwa kuwateua viongozi vijana kushikilia vyeo mbalimbali kwenye baraza la mawaziri.

“Rais amekuwa akiwaahidi vijana kwamba anatambua mchango wao lakini sasa ameonyesha hilo kwa vitendo,” akasema.

You can share this post!

Teuzi za mawaziri zagawanya jamii ya Wakalenjin

Wakuzaji kahawa Kirinyaga kufaidi ushirikiano na India

adminleo