Viongozi wapinga uuzaji wa viwanda vya sukari
DENNIS LUBANGAna BARNABAS BII
VIONGOZI kutoka maeneo yanayokuza miwa Magharibi mwa Kenya, wameitaka serikali kusimamisha shughuli za kubinafsisha viwanda vya sukari vilivyoko eneo hilo kutokana na changamoto za kiusimamizi na kifedha.
Badala yake, viongozi hao wanataka washikadau katika sekta hiyo kujadiliana na kutafuta suluhisho la kudumu kwa kampuni hizo, ili ziendelee kufanya kazi inavyofaa na kuhakikishia wakulima wa miwa kuwa watakuwa na soko la mazao yao na watakuwa wakilipwa muda ufaao.
Wakiongozwa na seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, viongozi hao walisema kuwa kuharakisha kubinafsisha kampuni hizo kutawasababishia wakulima wa miwa matatizo ya kiuchumi.
Walisema kamati iliyoundwa kuhakikisha viwanda hivyo vinabinafsishwa haijawahusisha viongozi wa eneo hilo.
“Inahuzunisha kuwa kamati iliyoundwa kuuza viwanda kama Nzoia inapanga kuviuza bila kuzungumza na viongozi ambao ndio wawakilishi wa wakulima,” akasema Bw Wetang’ula.
Vilevile, spika wa Seneti Kenneth Lusaka aliandikia usimamizi wa kiwanda cha Nzoia akiutaka kuharakisha malipo kwa madeni ya wakulima, ambao waliuzia kiwanda hicho miwa.
Bw Lusaka alishangaa ni kwa nini japo kiwanda chenyewe kimekuwa kikisaga miwa ya wakulima na kuuza sukari, hakijwalipa pesa zao.
“Sharti mambo yabadilike katika kampuni ya Sukari ya Nzoia wakati huu ambapo tuna usimamizi,” akasema Bw Lusaka.
Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa kampuni hiyo Joash Wamang’oli wiki iliyopita alitangaza kuwa bodi ilimteua Wanjala Makokha kuwa mkurugenzi wa kiwanda hicho, kufuatia kifo cha Michael Kulundu aliyeuawa na wakora mjini Bungoma, mnamo Januari 2.
Kumekuwa na madai kuwa usimamizi wa kiwanda hicho ulikuwa ukiwalipa watu wengine wanaokiuzia miwa, wakati wakulima wa eneo hilo wanaachwa nje, kwa kuwa wanaolipwa wamekuwa wakitoa hongo.
Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati aliitahadharisha serikali dhidi ya kuharakisha kubinafsisha viwanda vya sukari na kampuni zingine zilizoko eneo hilo, akiitaka kuachia serikali za kaunti kushiriki katika shughuli hizo kwa niaba ya wananchi.
“Kama serikali za kaunti tunafaa kuwa na usemi kwa niaba ya watu wetu kwa maelewano ya muda mrefu, ikiwa viwanda hivi vitauzwa,” Gavana Wangamati akasema.
Bw Wangamati pamoja na mwenzake wa Kisumu Anyang’ Nyong’o waliitaka serikali kuu kuzungumza na serikali za kaunti, ili kutafuta suluhu sitakazowazuia wakulima kutoumia, endapo viwanda hivyo vitabinafsishwa.