Habari Mseto

Viwanda vya humu nchini vyaanza kuunda barakoa

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

DENNIS LUBANGA na LEONARD ONYANGO

VIWANDA vya nguo vya humu nchini vimeanza shughuli ya kutengeneza barakoa kwa wingi katika juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Kiwanda cha nguo cha Rivatex East Africa Limited kilichoko Eldoret jana kilisema kuwa tayari kimeanza shughuli ya kutengeneza maski.Gavana wa Kitui Charity Ngilu naye alisema kuwa kiwanda cha Kitui County Textile Centre (Kicotec) kimeanza harakati za kutaka kutengeneza barakoa kwa wingi.

Barakoa hizo zinatarajiwa kusambazwa katika hospitali mbalimbali zinazotibu waathiriwa wa virusi vya corona.Huwa zinatumiwa kuepusha madaktari dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

Vilevile, huzuia waathiriwa kutosambaza virusi zaidi.Mkurugenzi Mtendaji wa Rivatex East Africa Limited Profesa Thomas Kurgat jana alisema kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kutengeneza maski 1,200 kwa siku.

Kulingana na Prof Kurgat, barakoa hizo zitasambazwa kwa madaktari ili kuwakinga dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Tayari tumetengeneza maski za kutosha kwa ajili ya wafanyakazi wetu. Sasa tumeanza kutengeneza maski zitakazosambazwa hospitalini. Tumechukua hatua hiyo kufuatia wito wa serikali wa kutaka viwanda kusaidia katika kupambana na virusi vya corona,” akasema Prof Kurgat.

Naye Gavana Ngilu alisema: “Kiwanda cha Kitui Kicotec kimejiandaa kikamilifu kutengeneza maski za kutosha. Tuendelee kufanya usafi na kufuata maelekezo ya serikali ili tujikinge na virusi vya corona.”

Wakati huo huo, kundi la mafundi wa nguo mjini Eldoret wamewavutia wakazi baada ya kutengeneza maski za bei nafuu.

Washonaji hao wa nguo wakiongozwa na Richard Rotara, walisema kuwa wanatengeneza barakoa 100 kwa siku.

Wanatumia vitambaa walivyoagiza kutoka nchini Uturuki kabla ya kutokea kwa mkurupuko wa virusi vya corona humu nchini.