Vyama viwe vikimchagua Rais, wabunge wapendekeza
LEONARD ONYANGO na WANDERI KAMAU
WABUNGE sasa wanataka Wakenya wasichague rais moja kwa moja, na badala yake wapigie kura vyama vya kisiasa.
Chama kinachopata wingi wa kura, kulingana na Spika Justin Muturi, kiteue rais pamoja na naibu wake.
Spika huyo wa Bunge aliyekuwa akihutubia Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) linaloongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji, alipendekeza magavana pamoja na manaibu wao pia wasipigiwe kura moja kwa moja.
“Ili kumaliza joto la kisiasa ambalo limekuwa likitanda kila wakati wa uchaguzi, tuondoe mfumo ambapo rais anachaguliwa na wapigakura. Vyama vipigiwe kura na kitakachoibuka na wingi wa kura kiteue rais pamoja na naibu wake,” akasema Bw Muturi.
Alisema mfumo sawa umekuwa ukitumiwa nchini Afrika Kusini ambapo chama kinachopata idadi kubwa ya kura wakati wa uchaguzi kinateua rais.
Nchini Afrika Kusini, kwa mfano, chama tawala cha ANC kimekuwa kikitwikwa jukumu la kuteua rais tangu nchi hiyo ipate uhuru 1994.
Mnamo 1994, chama cha ANC kiliteua Nelson Mandela kuwa rais baada ya kupata asilimia 63 ya kura zilizopigwa. Chama hicho pia kiliteua Thabo Mbeki (1997 – 2007), Jacob Zuma (2007 – 2017) na kiongozi wa sasa Cyril Ramaphosa.
Iwapo pendekezo hilo litatekelezwa na jopokazi la BBI, huenda likakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Naibu wa Rais William Ruto.
Dkt Ruto amekuwa akishikilia kuwa ni sharti rais achaguliwe moja kwa moja na wapigakura badala ya kuteuliwa na watu wachache.
Alipendekeza kila kaunti iwe ikichagua maseneta wawili; mwanamke na mwanaume. Hiyo inamaanisha Seneti itakuwa na maseneta 94 waliochaguliwa.
Bw Muturi pia anapendekeza mipaka ya maeneobunge ifutiliwe mbali na vyama viwe vikigawana viti vya ubunge kwa kuzingatia idadi ya kura.
Kiongozi wa Bunge la Kitaifa pia alipendekeza vyama vinavyokosa kiti bungeni viondolewe katika sajili ya vyama vya kisiasa.
Seneti nayo inataka ipewe jukumu la kuwapiga msasa mawaziri, ikiwa mawaziri hao watateuliwa kutoka Bunge la Kitaifa.
Maseneta walisema, itakuwa vigumu kwa wabunge kutwikwa jukumu la kuwapiga msasa watu wanaoteuliwa kutoka Bunge la Kitaifa, kwani watakuwa na ukaribu nao.
Wakiwasilisha mapendekezo yao mbele ya jopo la BBI jana, maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na James Orengo (Siaya) walisema Seneti yafaa ipandishwe hadhi kimajukumu, kama ilivyo Uingereza na Amerika.
Walisema chini ya mpangilio wa sasa, kuna mwingiliano mkubwa wa kimajukumu kati ya mabunge hayo mawili na hivyo haja ya kuyalainisha.
“Huwezi kutegemea wabunge kuwapiga msasa watu ambao wanateuliwa kama mawaziri miongoni mwao. Hilo litakuwa sawa na kuwapa nafasi kuwapiga msasa marafiki wao wenyewe,” akasema Bw Murkomen, ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti.