Habari Mseto

Wa Iria apendekeza mlo wa bure kwa wanavyuo vikuu

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na NDUNGU GACHANE

GAVANA wa Murang’a Mwangi wa Iria ametangaza nia ya kuanza mpango wa kutoa chakula bila malipo katika vyuo vikuu vya umma nchini, ili kuwawezesha wanafunzi kuangazia masomo kikamilifu.

Alitoa kauli hiyo kwenye hafla maalum ya kutia saini muafaka wa makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Murang’a na serikali ya kaunti hiyo kuhusu utoaji wa chakula kwa wanafunzi bila malipo.

Bw Wairia alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao bila matatizo, kwani imekuwa changamoto kwa wengi kupata chakula wanapoendelea na masomo.

Alishangaa kwa nini mfumo huo haujaanzishwa katika vyuo vikuu ikizingatiwa kuwa serikali huwa inatoa chakula cha bure kwa watu walio katika rumande, mahabusu na polisi makurutu. Alisema hilo halifai kwani wanafunzi hao ndio huchangia pakubwa katika ustawi wa nchi wanapomaliza masomo yao.

“Haifai wanafunzi wa vyuo vikuu kusahaulika, wakati serikali inatoa vyakula kwa mahabusu na polisi makurutu. Nitapigania hili kwa kila namna kupitia Muafaka wa Maridhiano (BBI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu,” akasema. Alieleza kuwa amefanya utafiti wa kina na kubaini kuwa wanafunzi wengi hukumbwa na ugumu mkubwa wa kupata chakula.

“Ikiwa tutaanza mpango wa kuwapa chakula wanafunzi, nina imani kwamba hali ya masomo itaimarika na wataboresha matokeo yao,” akaongeza.

Mwaka 2019 chama cha Civic Renewal Party (CRP) anachohusishwa nacho, kiliiomba Wizara ya Elimu kufutilia mbali mikopo ya Bodi ya Elimu ya Juu (Helb) kwa wanafunzi wote waliokamilisha hatua muhimu ya masomo yao lakini hawajaajiriwa.

Kulingana na chama hicho, wizara inapaswa kuwaondolea wanafunzi mikopo hiyo kutokana na changamoto nyingi zinazowakumba vijana nchini.

Alisema hilo linalingana na vile serikali ya kitaifa imeondoa mikopo kwa wakulima katika sekta za kahawa na majanichai.