Habari Mseto

Waajiriwa waponea padogo kuchomeka katika kiwanda

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

NAIBU Kamishna wa kaunti ndogo ya Makadara, Nairobi, Bw Fred Ndunga ameonya waajiri wanaowafungia wafanyakazi ndani ya viwanda vyao usiku kuwa watakamatwa.

Bw Ndunga alisema kumfungia mtu kazini na kwenda na funguo nyumbani ni ukiukaji wa haki za binadamu na pia kinyume cha sheria.

Bw Ndunga alikuwa akiongea na waandishi wa habari katika kiwanda cha Metro Plastics kwenye barabara ya Lunga Lunga, eneo la Viwandani kilichochomeka Jumamosi alfajiri.

“Zima-moto walifika haraka lakini shida ni kuwa kulikuwa na kemikali zilizoufanya kuzuka tena baada ya kuzimwa,” akasema. Yakisiwa mali ya thamani isiyojulikana iliteketea katika kisa hicho.

Baadhi ya wafanyakazi waliokuwa kazini moto ulipozuka walipata majeraha wakikanyangana na wengine kurukia juu ya kuta ili wajiokoe.

Bw Ndunga alisema maafisa wake wanachunguza picha za kamera za usalama (CCTV) ili kubaini ikiwa milango ya kiwanda hicho ilikuwa imefungwa..

Vilevile, nguzo za vyuma mahali palipotumiwa kama stoo na pengine palipoundiwa bidhaa zilikuwa zimeanguka.

Wakazi wa mtaa wa Lunga Lunga walilazimika kutoka kijijini kuepuka moshi mwingi uliowatatiza kupumua. Juhudi za kupambana na moto ziliwashirikisha wataalamu kutoka kampuni ya mafuta ya Kenya Pipeline na Kaunti ya Nairobi.