Habari MsetoSiasa

Wabunge wa Kisii sasa wanamtaka Matiang'i ajiuzulu

January 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka eneo la Gusii wanaoegemea mrengo wa Tangatanga wamemtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I kujiuzulu wadhifa wake na kujiunga na siasa ikiwa hatakoma kushirikiana wanaohujumu maendeleo katika sehemu hiyo.

Wakiongea na wanahabari Jumanne katika mkahawa wa Serena, Nairobi viongozi hao walimtaka waziri huyo kuungana nao katika vita dhidi ya ufisadi katika kaunti za Kisii na Nyamira.

“Inaudhi kuwa huku watu wetu wakiendelea kuumia kwa kukosa huduma na wanakandarasi kukosa kulipwa kwa sababu ubadhirifu wa pesa za umma na ufisadi, waziri Matiang’i anaendelea kuwalinda maafisa hao hao ambao anapaswa kuwachukulia hatua,” akasema Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro aliyesoma taarifa kwa niaba ya wenzake.

Aliandamana na wabunge; Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), Alfa Miruka (Bomachoge Chache) na Seneta Maalum Millicent Omanga. Vile vile, alikuwepo Mbunge wa Kuria Magharibi Mathias Robi na mwanaharakati wa kisiasa eneo la Kisii Don Bosco Gichana.

“Ikiwa Matiang’I ameshindwa na kazi yake kama Waziri wa Serikali basi hana budi kujiuzulu ili tupambane naye katika ulingo wa siasa. Kwa saaa tunamtaka apambane na maafisa wafisadi kulingana na agizo la Rais Uhuru Kenyatta aliyemteua kwa wadhifa huo,” akasema Bi Omanga.

Viongozi hao vile vile, walidai kuwa Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi anahangaishwa kwa kulaani ufisadi uliokithiri katika kaunti ya Kisii.

“Hii ndio maana Mheshimiwa Maangi sasa anasafiri kwa matatu baada ya kupokonywa magari yake rasmi kwa kupinga ufisadi. Juzi Ijumaa kabla ya kufanyika kwa mkutano wa BBI mjini Kisii alipokonywa magari na maafisa 12 wa polisi waliovamia kwake alfajiri,” akasema Bw Osoro.

“Ingawa Naibu Gavana amepiga ripoti kwa polisi kuhusu kisa hicho ambacho ni hatari kwa maisha yake, tunamtaka Waziri Matiang’i ahakikishe kuwa Bw Maangi ni salama,” akasema Bw Nyamoko.

Viongozi hao wametisha kuongoza maandamano katika kaunti za Kisii na Nyamira kulaani kile wanachodai ni utepetevu magavana James Ongwae (Kisii) na John Nyagarama (Nyamira).