Wabunge wa Pwani wataka serikali isaidie waathiriwa wa mafuriko
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wa Pwani wameitaka serikali ya kitaifa kutuma Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaidia wakazi wa eneo hilo ambao wameathirika na mafuriko kufuatia mvua iliyopitiliza inayoshuhudiwa eneo hilo.
Wakiongozwa na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi viongozi hao pia wameitaka serikali kusambaza vyakula vya msaada, dawa, mablanketi na vyandarua vya kuzuia mbu kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.
“Vilevile, tunaitaka serikali kutoa fedha kupitia Mamlaka ya Kusimamia Barabara za Mashambani (KeRRA) kwa ajili ya kukarabati barabara na madaraja ambayo yameharibiwa na mvua hii,” akasema Bw Mwinyi kwenye kikao na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge, Nairobi.
Aliandamana na wenzake, Ali Wario (Bura), Teddy Mwambire (Ganze), Mishi Mboko (Likoni), Ruweidha Obbo (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu) na Mbunge wa Malindi Kaskazini Owen Baya.
Wabunge hao pia wameitaka Wizara ya Elimu kufanya ukaguzi katika shule zilizoathirika na mafuriko ili kuzifanyia ukarabati kabla muhula wa kwanza kuanza Januari 2020.
“Uharibifu ambao kufikia sasa umesababishwa na mafuriko umeshinda uwezo wa serikali za kaunti na Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF). Hii ndiyo maana tunaomba serikali ya kitaifa iingilie kati ili watu wetu wasiendelee kuathirika,” akasema Bw Wario.