Habari MsetoSiasa

Wabunge wajadili kuvunja Seneti

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

VITA vya ubabe baina ya Bunge la Taifa na Seneti kuhusu lipi lina mamlaka zaidi, viliendelea bungeni Jumatano huku baadhi ya wabunge wakipendekeza Seneti ivunjwe.

Wito huo ulitolewa wakati Seneti inapotarajiwa kuwasilisha kesi kortini baada ya kukosa kuelewana na Bunge la Taifa kuhusu kiwango cha pesa ambazo zinafaa kugawiwa serikali za kaunti.

Wakijadili suala la tofauti baina ya mabunge hayo mawili, wabunge jana walikashifu Seneti wakidai imekuwa ikijitwika majukumu ya Bunge la Taifa.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed alidai Seneti inatambuliwa kikatiba kuwa bunge la kushughulika na “mambo madogo madogo” katika kaunti, na kuwa haina nguvu zozote.

“Bw Spika, Seneti inafaa kuvunjwa kwa kuwa hakuna kitu muhimu inafanya isipokuwa kuchukua kazi ambazo tayari zinafanywa na Bunge la Taifa,” akasema Bw Junet.

Alisema kuwa hata viongozi wa wengi na wachache katika Seneti hawafai kuwapo, na akatishia kufika mahakamani kupinga kulipwa marupurupu kwa viongozi hao, ambao sasa ni Kipchumba Murkomen wa wengi na James Orengo wa wachache, endapo Tume ya Huduma za Bunge (PSC) haitasitisha marupurupu wanayolipwa.

Wengi wa wabunge walidai kuwa Seneti inafaa kujikita katika masuala madogo kama ya makaburi, uokotaji wa takataka na masuala ya mifugo katika kaunti, wala si majukumu ya serikali kuu.

“Bw Spika Seneti inafaa kuvunjwa na ifanywe moja ya kamati katika Bunge la Taifa,” Mbunge wa Kathiani Robert Mbui akasema.

Wabunge walijitetea kuwa ndio wenye mamlaka ya kukagua utendakazi wa mashirika ya serikali kuu, na wakalaumu Seneti kuwa imekuwa ikiingilia majukumu hayo, kwa kuwaalika maafisa wa mashirika hayo, badala ya kushughulika na masuala yanayoathiri kaunti.

Lakini wakati huo huo, baadhi ya maseneta waliwajibu wakisema kuwa Seneti haiendi popote kwa kuwa imeundwa kikatiba.