Wabunge wamkejeli Sonko kuwabomolea wakazi nyumba
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Nairobi wamemshtumu Gavana wa Nairobi kufuatia kubomolewa kwa nyumba kadhaa mashariki mwa Nairobi baada ya mzozo wa ardhi.
Bw Benjamin Mwangi (Embakasi ya Kati) na Bi Mercy Gakuya (Kasarani) Alhamisi walitaja hatua ya Gavana Sonko kusimamisha ubomoaji huo kama “kutoa machozi ya mamba”.
“Mbona leo (Alhamisi) ndio anajifanya eti anaenda Kayole kusimamisha ubomoaji ilhali shughuli hiyo ilianza Jumanne. Hii ni kuwachekelea waathiriwa ambao wameishi nje kwa baridi baada ya nyumba kubomolewa na mali yangu kuporwa. Alikuwa wapi kuanzia Jumanne tingatinga zilipowavamia raia wasio na hatia?” akauliza Bw Mwangi, maarufu kama Meja Ndong’.
Bi Gakuya alisema kuwa Gavana Sonko alifahamu fika kuhusu mzozo huo na hivyo alipaswa kuchukua hatua za mapema kuzuia ubomoaji huo.
“Ikiwa gavana Sonko ni kiongozi anayejali masilahi ya wa Nairobi, basi angafanya juu chini kuzuia ubomoaji huo ambao umetekelezwa kinyama na kwa njia ambayo inakiuka haki za kibinadamu. Angeongea na maafisa husika katika serikali ya kitaifa ili kuzuia unyama uliotendewa watu wetu,” akasema Bi Gakuya.
Alhamisi Bw Sonko alizuru mitaa ya Kayole, Njiru na Mihango ambako ubomoaji huo uliendeshwa kuanzia Jumanne ambapo zaidi ya wakodishaji nyumba 6,000 waliathirika.
Gavana huyo alitangaza kusitishwa ubomoaji huo akisema amepata amri hiyo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.
“Hatuwezi kuzipokonya familia za Nairobi makao wakati ambapo wanatarajiwa kufurahia mazingira matulivu wakijiandaa kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya. Kwa hivyo, naamuru kwamba hakuna majengo mengine yatabolewa katika msimu huu wa sherehe,” Sonko akasema.
Lakini saa chache baada ya Sonko kutoa tangazo hilo, serikali ilitangaza kuwa imesitisha ubomoaji wa majengo yote nchini; ambayo yalijengwa katika maeneo yasiyohitajika. Maeneo hayo ni kando ya mito, eneo la upanuzi wa barabara na eneo la kupitishwa kwa nyaya za umeme.