Wabunge wapinga BBI kurudishwa kwa wananchi
Na SAMUEL BAYA
Wabunge watatu, wawili kutoka kaunti ya Nakuru na mmoja kutoka kaunti ya Baringo Jumapili walisema wako tayari kupitisha mapendekezo ya BBI kupitia bunge.
Katika mahojiano na Taifa Leo, wanasiasa hao walisema itakuwa makosa makubwa kurudisha tena mapendekezo hayo kwa wananchi ambao tayari walikuwa wametoa mapendekezo yao katika nyakati za awali kwa jopokazi la BBI.
Wabunge hao Dkt Daniel Tuitoek (Mogotio), Kuria Kimani (Molo) na Bi Charity Kathambi (Njoro) walisema hawaoni tatizo lolote kuunga mkono mapendekezo ya ripoti hiyo ya BBI kupitia kwa bunge.
Vile vile waliwalaumu wenzao wa upinzani kwa kuanza kugeuza mkondo wa majadiliano kuhusiana na ripoti hiyo ya BBI kwa kusema irudishwe tena kwa wananchi kutoa maoni yao.
Dkt Tutoek alisema kuwa haelewi ni kwa nini sasa wanasiasa wa ODM ambao ndio hasa waasisi wa mapendekezo hayo wanataka tena suala hili lirudishwe tena kwa wananchi ambao tayari walitoa mapendekezo yao katika nyakati za mwanzo.
“Mimi binafsi nikiwa chama cha Jubilee mwanzoni nilikuwa na shaka na mapendekezo haya, lakini baada ya mapendekezo haya kutolewa hadharani juzi, niliamua kuyaunga mkono. Ni kinaya kwamba ODM wenyewe sasa wamegeuka. Tatizo liko wapi. Naamini tukishirikiana sote pamoja, tutaipitisha,” akasema Dkt Tuitoek.
Alisema karatasi hiyo inahitaji tu kuundwa kwa sera na serikali kuhakikisha yale ambayo yametajwa katika ripoti hiyo yako sawa na yaantekelezwa. Haihitajika tena kurudishwa kwa wananchi.
Mwito wake uliungwa mkono na mbugne wa Molo Bw Kuria Kimani kwamba hakuna haja ya ripoti hiyo kurudishwa tena mashinani.
“Kwanini turudishe tena mapendekezo hayo kwa wananchi wakati ambapo walitoa maoni yao. Takribani nusu ya mapendekezo yote yanahusisha uundwaji wa sera za kitaifa kuyashughulikia na sio vyenginevyo,” akasema Bw Kimani.
Naye mbunge wa Njoro Bi Charity Kathambi alisema atahakikisha kwamba ameendeleza kampeini zake vijijini ili kuhakikisha kwamba wananchi wamesoma mapendekezo hayo na kuelewa ajenda zake kuu.
Alisema kuwa kuna haja ya wakenya kusoma mapendekezo ya kikosi kazi hicho cha BBI na kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya baadaye ya maisha yao kaka wakazi wa Njoro.
Alikuwa akiongea baada ya kufungua daraja la Njokerio katika eneobunge lake.
“Kutolewa wazi kwa ripoti hiyo kulimaliza misisimuko iliyokuwapo kuhusiana na jopo kazi hilo. Jambo ambalo tunataka sasa ni nyinyi kama wakazi wa Njoro musome kwa makini mapendekezo hayo kisha mufanye maamuzi,” akasema Bi Kathambi.