• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wachache wajitokeza kuadhimisha siku ya Leba Dei

Wachache wajitokeza kuadhimisha siku ya Leba Dei

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI na wananchi jana walisusia sherehe za Leba Dei katika maeneo mbalimbali nchini, huku baadhi ya wafanyakazi wakidai hakukuwa na chochote cha kusherehekea.

Katika kaunti kadha nchini ni viongozi wa chache wa vyama vya wafanyakazi na maafisa wa serikali ambao walifika katika viwanja mbalimbali ambako sherehe hizo zilifanyika, huku wananchi na viongozi wa matabaka mbalimbali wakikosa kuonekana.

Katika kaunti ya Mombasa, viongozi wakiwemo Gavana Hassan Joho, Seneta Mohammed Faki, wabunge na madiwani hawakufika katika uwanja wa Tononoka ambako sherehe hizo zilifanyika.

Mwakilishi wa Muungano wa Wafanyikazi Nchini (COTU) katika kaunti hiyo, Bw Gideon Mutiso aliwakashifu viongozi hao kwa kususia sherehe hizo akisema haja yao kubwa huwa ni “kuwahadaa wakazi hasa wakati wa kuomba kura”.

“Kwa kususia sherehe hizo, viongozi hao wanaonyesha wazi kuwa hawajali maslahi ya wafanyakazi kwani hata hawajawahi wasilisha mswada wowote unaotetea masilahi ya wafanyakazi hao,” alisema Bw Mutiso.

Magharibi mwa Kenya, sherehe hizo zilifeli kufanyika katika baadhi ya kaunti kama vile Kakamega na Homa Bay kutokana na kile kilichotajwa kama ukosefu wa fedha.

Na katika kaunti ya Kisii watu wasiozidi 100 ndio walihudhuria sherehe hizo katika uwanja wa michezo wa Gusii, huku gavana wa Kisumu, Prof Peter Anyang’ Nyong’o,  akiahidi kuhakikisha kuwa anazingatia usawa katika uajiri wa wafanyakazi katika serikali yake.

Gavana wa Bomet, Dkt Joyce Laboso alikosa kuhudhuria sherehe hizo katika eneo bunge la Konoin. Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na naibu wake, Bw Hillary Barchok, Dkt Laboso alizitaka kampuni za majani chai katika sehemu hiyo kutowafuta kazi wafanyakazi baada ya kuanzisha mtindo wa kutumia mashine katika uchumaji wa zao hilo.

Na katika kaunti ya Nakuru ni watu wachache mno waliohudhuria sherehe za Leba Dei katika uwanja wa michezo wa Afraha.

Na hawakutumbuizwa kama ambavyo imekuwa kawaida katika Siku Kuu za Kitaifa ambazo hufanyika katika uwanja huo.

Bw Francis Makokha ambaye ndiye alikuwa mshirikishi wa sherehe hizo alisema ilifanikiwa licha ya kuvutia idadi ndogo ya watu, haswa wafanyakazi.

“Ningependa kuwakashifu vikali waajiri ambao walikataa kuwapa nafasi wafanyakazi wao kuhudhuria sherehe hii yenye umuhimu mkubwa,” akasema Bw Makokha ambaye ni afisa wa Wizara ya Leba katika kaunti ya Nakuru.

Ripoti ya Anthony Kitimo, George Odiwour, Benson Amadala, John Njoroge na Jadson Gichana , Victor Otieno, Vitalis Kimutai na Charles Wasonga

You can share this post!

Kaunti ya Nairobi kutumia Sh100 milioni kuangamiza mbwa...

Kalonzo ataka sheria kuhusu utajiri wa viongozi ibuniwe

adminleo