Habari Mseto

Wadau kuandaa kikao kutatua migogoro kuhusu ukuzaji miraa

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na DAVID MUCHUI

MASHIRIKA mbalimbali ya serikali yamepanga kukutana na washikadau wengine kushughulikia masuala tatanishi yanayolemaza kunawiri kwa sekta hiyo.

Mkutano wa siku mbili wa wadau utafanyika Nairobi kuanzia leo.

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni kuhusu uorodheshaji wa miraa kama dawa ya kulevya, athari za miraa kwa afya na pia sheria za kaunti tofauti kuhusu miraa.

Mwenyekiti wa jopokazi la utekelezaji wa ripoti kuhusu miraa, Bw Kello Harsama alialika idara na mashirika zaidi ya kumi ya kiserikali.

Baadhi ya walioalikwa ni maafisa wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Kenya (KEMRI), Wizara ya Biashara, Shirika la Kitaifa la Kupambana na Uraibu wa Dawa (NACADA) na Idara ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS).

Wengine ni kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Kenya (KRA) na Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege Kenya (KAA).

“Tumepokea mapendekezo kadhaa kutoka kwa wadau wakuu lakini kuna masuala mazito ambayo bado yana utata kwani mashirika ya serikali yameshikilia misimamo mikali,” akasema Bw Harsama kwenye barua kwa wakuu wa mashirika husika.