Habari Mseto

Wafanyabiashara wadogo kuendelea kuumia

July 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

HUENDA wafanyabiashara wadogo nchini wakakosa kupata afueni licha ya hatua kadhaa za kufungua uchumi zilizotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu.

Miongoni mwa hatua alizotangaza Rais ni kuondolewa kwa marufuku ya usafiri kutoka ama kuingia katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera.

Ingawa ni hatua inayoonekana kuimarisha hali ya uchumi ambao umedorora, wadadisi wa kiuchumi wanasema wale ambao watapata afueni kiasi ni wahudumu wa sekta ya usafiri na utalii.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, mdadisi wa masuala ya uchumi Tony Watima, alisema safari bado ni ndefu kwa wanaofanya biashara ndogo ndogo, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta hakuondoa kafyu ambayo imekuwepo tangu Machi.

“Hakuna afueni yoyote ya haraka kwa wenye biashara ndogo ndogo. Wale ambao walifaidika kutokana na hotuba hiyo ni watu wanaohudumu katika sekta za uchukuzi na utalii. Wafanyabiashara wanaotoa huduma zinazowiana na sekta hizo ndio watakaopata afueni, japo si haraka kwani janga lingali nasi,” akasema Bw Watima.

Kuhusu kuongezwa kwa marufuku ya mitumba, wadadisi wanasema hilo litaendelea kuwaathiri wafanyabiashara wa kiwango cha chini, kwani wengi hutegemea mapato kutoka uuzaji wa nguo hizo kupata riziki.

Kulingana nao, suluhisho kuu litapatikana tu wakati vizingiti vyote vilivyowekwa vitakapoondolewa.

Kulingana na takwimu za Halmashauri ya Kukusanya Takwimu Kenya (KNBS), karibu Wakenya milioni moja wamepoteza ajira zao tangu janga hilo kuanza mnamo Machi.

Ripoti za mashirika kadhaa kama Infotrak na TIFA pia zimetabiri kuwa hali ya uchumi itachukua muda kabla ya kurejea ilivyokuwa.