• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
UFISADI: Wafanyakazi 18 wa Kenya Power wapigwa kalamu

UFISADI: Wafanyakazi 18 wa Kenya Power wapigwa kalamu

Na CECIL ODONGO

WAFANYAKAZI 18 wanaoshukiwa kuhusika na utoaji zabuni kwa mapendeleo katika kampuni ya umeme ya Kenya Power, wamefutwa kazi kufuatia uchunguzi wa ndani uliofanywa.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Bw Ken Tarus Jumatatu alisema kwamba kampuni hiyo iliamua kuwafuta kazi wafanyakazi hao baada ya kufanya uchunguzi wa ndani.

“Tulitafuta huduma za wanakandarasi 500 lakini kukaibuka malalamishi kwamba zaidi ya 350 walipata tenda hizo kutokana na uhusiano wao na wafanyakazi wetu wala siyo kuhitimu kwao. Tulianzisha uchunguzi wetu na kati ya 19 waliodaiwa kuhusika 18 walipatikana na hatia na tayari tumewatimua,” akasema Bw Tarus.

Aidha murugenzi huyo aliikaribisha hatua ya ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma ya kutaka kufanya uchunguzi wao kuhusu sakata hiyo japo akakiri hawajapata barua kutoka kwa ofisi hiyo kuthibitisha hayo.

Bw Tarus alidai kwamba waliopatikana na hatia waliwapa zabuni jamaa na marafiki wao kinyume na sheria ya maadili ya kikazi inayomzuia mfanyakazi kupata wala kumpa jamaa zake kandarasi za utoaji huduma katika kampuni ya KPLC.

Hata hivyo alisisitiza kwamba uchunguzi unaoendeshwa kahusu sakata hiyo haihusu kupotea kwa fedha jinsi inavyosawiriwa machoni pa umma bali unauhusu mchakato mzima wa utoaji zabuni uliojaa utata.

Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza katika kikao na wanahabari kilicholenga kutoa mwanga kuhusu sakata hiyo katika Jumba la Electricity jijini Nairobi.

Pia aliwaondolea hofu wateja wao kwa kusisitiza kwamba malalamishi yao kuhusu ongezeko la bili za stima yametatuliwa kwa kiasi kikubwa na kesi chache zinazosalia zinaendelea kutatuliwa.

You can share this post!

Korti yaruhusu serikali kujenga nyumba 7,000

Mkasa wa Solai: KHRC yalaumu taasisi za serikali

adminleo