Wafanyakazi hewa wamemumunya Sh300m Nyamira – Ripoti
NA RUTH MBULA
KAUNTI ya Nyamira imewalipa wafanyakazi hewa zaidi ya Sh300 milioni kwa kipindi cha miaka minne iliyopita kulingana na ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha za kaunti hiyo.
Ripoti hiyo tayari imekabidhiwa Gavana John Nyagarama ambaye anatarajiwa kuiwasilisha kwa wawakilishi wadi wa kaunti ili ipitishwe kisha mapendekezo yake yatekelezwe kikamilifu.
Ilibainika kwamba maafisa wakuu wa kaunti, kwa ushirikiano na jamaa za gavana huyo ndio wamekuwa wakihusika na uporaji huo na wafanyakazi kupandishwa vyeo kwa njia isiyofaa, kuwasilisha malimbikizi ya mishahara na kuwaajiri wafanyakazi hewa.
Bw Nyagarama ndiye aliagiza ukaguzi huo ufanyike katikati ya mwaka huu baada ya kubainika kwamba kaunti hiyo ilikuwa na wafanyakazi hewa zaidi ya 1,000.
Ingawa hivyo, Bw Nyagarama ameahidi kwamba sheria itachukua mkondo wake na hata jamaa zake wanaodaiwa kuhusika hawatasazwa.
“Hakuna mtu atakayesazwa na kila mtu awe alikuwa ameajiriwa au la ataadhibiwa vikali iwapo itabainika alichangia ukora huu ambao umesababishia kaunti hasara kubwa,” akasema Bw Nyagarama.
Katika kisa kimoja, mwanafunzi alipokea barua ya kuajiriwa hata kabla kumaliza masomo yake ya kidato cha nne. Barua ya kupewa kazi iliandikwa Aprili 2019 ilhali cheti chake cha KCSE kiliandikwa Novemba 2016.
Katika kisa kingine cha kushangaza, mfanyakazi wa kaunti aliyeajiriwa 2014 alikwea ngazi kwa kipindi cha miaka minne na kuwa kati ya maafisa wanaolipwa fedha nyingi na serikali ya kaunti hiyo.
Cha kushtusha ni kwamba, wafanyakazi ambao walipewa kazi kupitia utaratibu usiofaa walilipa zaidi ya Sh100,000, wengi wao wakiwa waendeshaji wa bodaboda.