Habari Mseto

Wafugaji kuku Kiambu waililia serikali iwaokoe

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Gakui, Gatundu Kaskazini wanalalamikia kufifia kwa biashara ya ufugaji wa kuku.

Wakulima hao chini ya mwavuli wa Kiambu Poultry Farmers Association wanatoa mwito kwa serikali kuingilia kati ili kuokoa biashara ya ufugaji wa kuku.

Mfugaji mashuhuri Bw John Njenga alisema biashara yake imedorora kwa kiwango kikubwa ambapo hata kupata soko la kuuza mayai ni taabu.

Anaeleza kuwa kwa muda wa mwaka mmoja sasa biashara hiyo imekuwa ni ya kubahatisha kila mara huku akikadiria hasara kubwa ajabu.

“Hapo awali nilikuwa nikiuza mayai zaidi ya 5,000 kwa wiki lakini kwa sasa ninauza 500 pekee. Biashara hii inatuletea hasara kubwa,” alisema Bw Njenga.

Alisema wakati mwingine analazimika kuchuuza mayai hayo vijijini kwa bei ya chini sana.

Alieleza jinsi chakula cha kuku kimeongezwa bei maradufu na ndio maana wanaililia serikali kuingilia kati ili kuhakikisha mfugaji wa kawaida amenufaika na jasho lake.

“Jambo linaloponza juhudi zetu zaidi ni bidhaa kama mayai na maziwa ambazo huingizwa hapa nchini kwa bei ya chini. Hii ni hatari kwa mfugaji wa kawaida kwa sababu hakuna wakati atafadika kwa vyovyote vile,” alisema Bw Njenga.

Alisema bei ya dawa ya kutibu kuku iko juu na kwa mkulima wa mashinani huo ni mzigo mkubwa kwake.