Habari Mseto

Wahalifu Kiandutu wapewa ilani ya saa 24 kusalimisha bunduki walizo nazo

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kiandutu, mjini Thika, wamepewa muda wa saa 24 pekee kusalimisha bunduki walizo nazo.

Kamanda mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Kiambu, Bw Ali Nuno, alisema Jumanne tayari ana habari ya kwamba wahalifu fulani wanamiliki bunduki katika kijiji hicho.

“Ninatoa amri kwa wakuu wa polisi mjini Thika wafanye hima kutafuta silaha hizo kabla sijafikiria hatua nitakayochukua,” alisema Bw Nuno

Alisema yeye kama kinara wa maswala ya usalama katika himaya ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, hatakubali hali ya usalama kuzorota.

Alizidi kusema ya kwamba Kaunti ya Kiambu ina idadi ya watu wapatao 3.5 milioni na kwa hivyo hali ya usalama ni sharti iimarishwe kwa sababu eneo hilo liko karibu zaidi na jiji la Nairobi.

Alisema hali ya kulinda usalama kupitia njia ya Community Policing, imezorota sana katika eneo la Thika na vitongoji vyake.

“Hata hivyo, maeneo ya Lari, Kikuyu, na Kiambaa hali ni ya kuridhisha kwani walinda usalama, polisi na wananchi wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa,” alisema Bw Nuno.

Alisema atahakikisha anaangamiza uhalifu katika Kaunti hii ya Kiambu jinsi alivyofanya wakati alikuwa akihudumu kama mkuu wa Polisi sehemu za Kayole Nairobi, na Nyeri mkoa wa kati.

Hamasisho

Aliyasema hayo alipokutana na wahudumu wa bodaboda wapatao 600 wa mji wa Thika waliofika Uwanja wa Starehe, Thika kuhamasishwa kuhusu usalama na kuweka nidhamu.

Hawa ni baadhi ya wahudumu wa bodaboda waliohudhuria mkutano kuhusu usalama uliyofanyika katika uwanja wa Community, Starehe, Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwashauri wanabodaboda kufanya juhudi kuona ya kwamba wanastahili kuwa na chama – wote wanaohudumu – kwa sababu ya kuhifadhi mambo yote muhimu kutoka kwa kila mmoja.

“Kila mwanabodaboda ni sharti awe na namba yake ya usajili na itundikwe mgongoni mwake ili mteja wake aweze kumtambua wakati wowote anapobebwa naye,” alifafanua Bw Nuno.

Alisema hakuna Polisi yeyote yule ana ruhusa kumnyanyasa mwanabodaboda yeyote bila sababu.

“Iwapo nitapata habari kuwa afisa yeyote wa polisi amemdhulumu mwanabodaboda yeyote bila shaka hatua kali itachukuliwa mara mmoja bila kujali wewe ni nani,” akaelezea Bw Nuno.