Habari Mseto

Wahasiriwa wa bomu katika ubalozi wa Amerika jijini Nairobi walilia haki miaka 26 baadaye

Na RICHARD MUNGUTI, LABAAN SHABAAN December 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JAJI Lawrence Mugambi amemwagiza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, kitengo cha kuamua kesi za ukiukaji wa haki za binadamu, asake faili saba za wahasiriwa wa mlipuko wa bomu ulioua watu zaidi ya 200 katika Ubalozi wa Amerika jijini Nairobi mnamo Agosti 7, 1998.

Jaji Mugambi alitoa agizo hilo Jumanne kufuatia ufichuzi kwamba faili saba zimetoweka.

Mawakili wa Kampuni ya Sheria ya Dkt John Khaminwa na John Mwariri walishtaki serikali wakitaka iwalipe fidia wahasiriwa hao.

“Hatutaendelea na kesi hii ikiwa faili saba za korti kuhusu kesi hii hazipo mbele ya mahakama,” wakaapa.

Dkt Khaminwa alidai kuwa wafisadi wamevamia mahakama  na kuiba faili za wahasiriwa hao.

“Huenda Al-Qaeda wameivamia mahakama na kuiba faili za wahasiriwa jinsi walilipua ubalozi wa Amerika Agosti 7, 1998,” Dkt Khaminwa alisema.

Wakili huyo alisema watu wengi kati ya 5,000 waliojeruhiwa, wameaga dunia kabla ya serikali kuwalipa fidia.

Wakili Dkt John Khaminwa (kulia) anawatetea wahasiriwa wa mlipuko wa bomu kortini jijini Nairobi mnamo Jumanne Disemba 3, 2024. Picha|Richard Munguti

Dkt Khaminwa alisema ni jambo la kusitikisha sana kuwa, badala ya serikali kuwafidia wahasiriwa, imeendelea kuwanyanyasa.

Wakili huyo alisema watu 600 walioshtaki serikali wamekuwa wakifika kortini na kurudi bila kupata haki.

“Baadhi ya wahasiriwa hawa wameumia mno na hata wengine walijeruhiwa katika sehemu za siri kutokana na mlipuko huo wa bomu,” Dkt Khaminwa alisema.

Wakili huyo mkongwe alieleza korti kwamba mateso wanayopitia waathiriwa hao ni magumu.

Jaji Mugambi aliamuru kesi hiyo ianze kusikizwa Aprili 10, 2025.

Pia aliamuru msajili wa mahakama afike kortini Februari 27, 2025 kuripoti ikiwa amepata faili hizo.