Habari Mseto

Wahisani walivyochanga Sh2m katika saa chache kwa vijana waliouawa na polisi

Na HILARY KIMUYU June 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MCHANGO ambao ulikuwa unaendeshwa kwa ajili ya vijana wawili walioongoza maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024, wiki iliyopita,  Jumapili ulitinga Sh2 milioni.

Pesa hizo ambazo zilichangishwa kwa muda wa saa nane zilikuwa za Rex Kanyeki Masai, 29 ambaye aliaga dunia mnamo Alhamisi wiki jana kutokana na majeraha ya kupigwa risasi.

Pia pesa hizo zilikuwa zikichangiwa Evans Kiratu, 21 ambaye aliaga dunia baada ya kugongwa na mkebe wa gesi ya kutoa machozi aliorushiwa kwenye sehemu nyeti wakati wa maandamano.

Kufikia Jumapili jioni, mchango huo ulikuwa umefikisha Sh2, 342, 830 na ulikuwa umetumwa na watu 6,486.

“Rex na Evans walituunga mkono katika kila jambo na sasa ni wakati wa kuzisaidia familia zao. Jiunge nasi ili kuwasaidia kuwapa mazishi ya heshima,” ujumbe kutoka M-Changa ukasema.

“Pesa hizo zitagawanywa kwa usawa kati ya familia ya Masai na Kiratu,” ikaongeza ujumbe huo.

Rex jinsi alivyojulikana, aliaga dunia baada ya kufikishwa katika Kituo cha Afya cha Bliss barabara ya Moi Avenue.

Tukio hilo lilijiri wakati wa maandamano Nairobi Alhamisi wiki jana ambapo vijana walijibwaga barabarani kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Mswada huo utapigiwa kura mnamo Jumanne baada ya wabunge 204 dhidi ya 105 kuupitisha uliposomwa kwa mara ya pili bungeni wiki jana.

Kiratu naye alikimbizwa hadi Hospitali ya Kenyatta na msamaria mwema baada ya kupatikana amejeruhiwa barabarani. Anatoka Kiambu na alikuwa ameacha kuishi na wazazi wake na kuanza maisha kivyake mwezi moja uliopita.