• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
‘Wahudumu 526 wa afya wameambukizwa corona’

‘Wahudumu 526 wa afya wameambukizwa corona’

Na SAMMY WAWERU

Wahudumu wa afya wapatao 526 ndio wameambukizwa Covid-19 kufikia sasa, imethibitisha Wizara ya Afya Jumatatu.

Wizara imetoa takwimu hizo siku chache baada ya wahudumu wa afya 41 katika Hospitali ya kujifungulia akina mama ya Pumwani, Nairobi kupatikana na virusi vya corona.

Wakati huohuo Wizara ya Afya imesema vituo vya afya nchini vinaendelea kupokea na kulaza wagonjwa wanaopatikana na corona na ambao hali yao haiwaruhusu kutunziwa na kutibiwa nyumbani.

“Sababu ya kuzindua mpango wa matunzo na matibabu ya nyumbani ni kuondoa msongamana katika vituo vya afya hasa kwa wasioonyesha dalili za Covid-19 licha ya kupatikana kuugua, ili kupata nafasi ya kulaza waliolemewa,” akasema Dkt Rashid Aman, Waziri Msaidizi katika wizara.

Alisema mikakati ya kuhakikisha kila kaunti ina vituo vyenye vitanda visivyopungua 300 kulaza wagonjwa waliozidiwa na homa ya corona inaendelea.

Dkt Aman alisema serikali imeona mafanikio katika mpango wa matunzo ya wagonjwa wa virusi vya corona nyumbani, ambapo idadi kubwa ya wanaopona imeshuhudiwa.

“Wanaoshughulikiwa nyumbani, ni wasioonyesha dalili za maambukizi licha ya kuthibitishwa kuwa na COVID-19,” Waziri akasisitiza.

Anakotunziwa mwathiriwa, lazima kuwe na nafasi ya kutosha ambapo anatakiwa kuwa na choo na bafu yake binafsi ili kuepuka kuambukiza wengine corona.

Wizara ya Afya imetoa maelezo zaidi kwenye mtandao wake wa tovuti jinsi ya kutunza waathiriwa nyumbani.

Vilevile, kuna wahudumu wa afya wa kijamii wa kujitolea waliotwikwa jukumu na serikali kufuatilia hali ya wagonjwa.

Wakati huo huo, serikali ilisema takwimu za maambukizi ya virusi vya corona hazijaborongwa.

Dkt Aman amewataka Wakenya kuwa na imani na serikali, badala yake akiwahimiza kutilia mkazo sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti kuenea kwa corona.

Alieleza kushangazwa na watu kutilia shauku takwimu zinazotolewa, wakati ambapo maambukizi yanazidi kuongezeka kila uchao.

“Tusiwe kama akina ‘Thomas’ wanaotilia shaka kila kitu, hata yale yanaonekana wazi ni ya kweli. Tusisubiri hadi pale tutaathirika moja kwa moja, lazima tuheshimu sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia ugonjwa huu kuenea zaidi,” akasema.

Waziri alitoa kauli hiyo kutokana na tetesi za baadhi ya Wakenya kwamba idadi ya visa vinavyotangazwa nchini si sahihi.

Aidha, Dkt Aman alisema kutokana na kuendelea kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya Covid-19, wananchi wajue “mambo si mazuri”, na kwamba kuna haja ya kila mmoja kuchukua tadhari kujizuia kuambukizwa na kuzuia wengine kwa kutilia maanani mashauri yaliyotolewa na wizara ya afya.

“Idadi tunayoona inapaswa kututia wasiwasi. Tunahitaji kupambana kudhiti maambukizi. Inaonekana ujumbe haujokolea akilini mwa watu, katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia idadi ya visa ikiongezeka kwa kasi, ilhali baadhi ya watu na hata viongozi wanafanya utani,” akaonya.

Kufikia sasa, Kenya imeandikisha zaidi ya visa 13,700 vya maambukizi ya Covid-19.

Waziri Aman alisisitiza, kasi ya maambukizi itadhibitiwa iwapo kila mwananchi atatii sheria na mikakati iliyowekwa.

Wakati akitoa takwimu za Jumatatu, mkanganyiko wa idadi ya waliofariki kutokana na corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita uliibuka, ambapo Dkt Aman alikuwa ametangaza kwamba wagonjwa 19 ndio wamethibitishwa kufariki , akisema idadi hiyo imefikisha jumla ya 258 walioaga dunia.

Waandishi wa habari ndio waliibua maswali, wakilinganisha takwimu hiyo na ya mnamo Jumapili. Waziri hata hivyo alirekebisha na kutangaza kuwa wagonjwa 4 ndio wamefariki na kufikisha jumla ya 238 walioangamizwa na Covid-19.

You can share this post!

Mikahawa sasa inauza pombe – Serikali

Mkazi ashangaza wanakijiji kufukuza mkewe aishi na mume...

adminleo