Wahudumu wa boti wataka LAPSSET iwafidie
NA KALUME KAZUNGU
WAHUDUMU wa boti na mashua kaunti ya Lamu wanaitaka serikali kupitia halmashauri ya bodi ya usimamizi wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) kuwafidia.
Hii ni kutokana na kile wanachodai kuwa ni kuathiriwa kwa njia zao za usafiri, jambo ambalo wanasema huenda likapelekea wengi wao kuacha kazi zao punde bandari ya Lamu itakapoanza kutekeleza shughuli zake eneo hilo.
Mradi wa Lapsset unajengwa eneo la Kililana, Kaunti ya Lamu.
Katika mahojiano na Taifa Leo mjini Lamu Jumatatu, Mwenyekiti wa wahudumu wa boti na mashua kaunti ya Lamu, Hassan Awadh, alisema takriban asilimia 80 ya wahudumu wa vyombo vya baharini wataathiriwa na shughuli za LSPSSET.
Kaunti ya Lamu ina wahudumu wa boti zaidi ya 5000.
Bw Awadh alisema huku LAPSSET ikifanya makadirio na kuwafidia wavuvi walioathiriwa na mradi huo, pia ni bora kwa wahudumu wa mashua na boti kushirikishwa na kufahamishwa ni jinsi gani watafidiwa kufuatia athari zinazotokana na LAPSSET.
“Hapa kisiwani Lamu pekee tuko na wahudumu 375 wa boti na mashua ambao wamesajiliwa kwa chama chetu lakini tukijumulisha visiwa vingine, tuko na zaidi ya wahudumu 5000. Ombi letu kwa LAPSSET ni kuhakikisha tumeshirikishwa na pia kufahamishwa ni jinsi gani tutafidiwa baada ya shughuli zetu kuathiriwa na Lapsset punde itakapoanza kufanya kazi.
Cha msingi ni kwamba tulipwe fidia zetu sawia na wavuvi wenzetu walioathiriwa na bandari. Huenda wengi wetu tukalazimika kuacha kazi zetu kwani Lapsset itapelekea baadhi ya njia zetu baharini kufungwa,” akasema Bw Awadh.
Wahudumu hao wa boti na mashua aidha walionya kwamba watashiriki maandamano iwapo LAPSSET haitatii matakwa yao na kuwafidia.