• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Wahusika katika sakata ya nepi za watoto mashakani

Wahusika katika sakata ya nepi za watoto mashakani

NYABOGA KIAGE na STELLA CHERONO

IDARA ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa uhalifu(DCI) imewaamrisha maafisa wa Shirika la kukadiria ubora wa bidhaa(KEBS), maajenti wa kuidhinisha upitishaji wa mizigo, wasafirishaji na duka maarufu la Mlolongo Eens Go-down kufika mbele yake baada ya kupatikana kwa tani tano za nepi za watoto zilizopitisha tarehe ya kuuzwa.

Makachero waliwafumainia wafanyakazi wa duka hilo Jumamosi wakipakia na kuzipa brandi mpya nepi hizo ili kuficha tarehe ya mwisho ya kuuzwa ambazo ni kati ya mwezi Januari na Mei mwaka 2017.

Alipogundua kwamba kulikuwa na njama ya kuficha uhalifu huo na kukingwa kwa mmiliki wa duka hilo ambayo ni mfanyabiashara maarufu, mkurugenzi wa DCI George Kinoti alimwaamrisha DCIO wa Parklands David Chebii kusimamia uchunguzi kuhusu ukora huo.

“Nepi hizo zilikuwa zimepita tarehe ya kuuzwa na zilikuwa zikipakiwa upya ili ukora huo usigunduliwe. Hii ni hatari sana kwa watoto wetu wasiokuwa na hatia,” akasema Bw Kinoti.

Wafanyakazi sita waliofumaniwa wakipakia nepi hizo walikamatwa huku polisi wakilazimika kuvunja mlango wa duka hilo ili kuendeleza uchunguzi baada ya mmiliki wake aliyekuwa na ufunguo kukosa kujitokeza kulifungua.

Nepi hizo baadaye zilipakiwa ndani ya lori na kusafirishwa hadi ofisi ya DCI katika barabara ya Kiambu.

Bw Chebii alisema wafanyakazi walionaswa walikuwa wakizipakia kisha kuweka nembo feki za Kebs kuficha tarehe ya matumizi na pia kubadilisha nembo ya kampuni iliyotengeneza nepi hizo kutoka Fujian Hanhe Sanitary products Company Limited hadi Eeze Life Products Limited.

“Bidhaa hizo baada ya uchunguzi wetu ziliingizwa nchini kimagendo miezi mitatu iliyopita na wafanyakazi hao walikuwa wakizitia muhuri iliyona tarehe isiyo sahihi ya kukamilika kwa muda wa matumzi,” akasema Bw Chebii.

Wakati wa oparesheni hiyo polisi pia walinasa machine zilizokuwa zikitumka kubadilisha tarehe na nembo za nepi hizo.

Kufuatia oparesheni hiyo, idara ya DCI imewatuma makachero katika miji ya Mombasa na Athi River kuchunguza jinsi nepi hizo zilivyoingizwa nchini bila kujulikana wakishuku kwamba kulikuwa na ushirikiano kati ya waagizaji haramu wa bidhaa na wafanyakazi wa KEBS katika bandari ya Mombasa.

You can share this post!

Maafisa wa serikali waliohepa Mashujaa Dei pabaya

NEMA yanasa mifuko ya plastiki kutoka Tanzania

adminleo