Waiguru aondoka, Abdullahi akiingia CoG huku magavana wa kike akichemkia matokeo ya kura
GAVANA wa Kaunti ya Wajir Ahmed Abdullahi, Jumatatu alichaguliwa kama mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana na kuchukua nafasi ya mwenzake wa Kirinyaga, Anne Waiguru.
Hatamu ya Waiguru ilifika kikomo baada ya kuhudumu kwa mihula miwili kama kiongozi wa baraza hilo.
Uchaguzi huu ulifanyika muda mfupi kabla ya hotuba kuhusu hali ya ugatuzi iliyotolewa katika Safari Park Hotel, Nairobi.
Mkuu wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga, sasa ndiye naibu mwenyekiti mpya wa CoG akijaza nafasi iliyoshikiliwa na Gavana Abdullahi.
Kinyang’anyiro cha mwenyekiti mpya wa CoG kilivutiwa ushindani mkali baina ya magavana watano akiwemo Johnson Sakaja (Nairobi), Joseph Ole Lenku (Kajiado), Abdullahi (Wajir), Kahiga (Nyeri) pamoja na Muthomi Njuki (Tharaka Nithi).
Hata hivyo, magavana wanawake hawakufurahishwa na hatua ya magavana kukosa kuteua mkuu wa kaunti mwanamke kama mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa baraza hilo, huku wakifululiza nje ya chumba ambapo matokeo ya uchaguzi yalitangazwa.
Ghadhabu yao ilichochewa zaidi wakati kwa viti vyote 21, ni gavana mmoja tu mwanamke, Wavinya Ndeti (Machakos), aliyechaguliwa kuhudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Biashara na Vyama vya Mashirika.
Nyadhifa zilizosalia 17 za wenyekiti zilitwaliwa na magavana wanaume. Wadhifa wa kiranja wa CoG ulitwaliwa na Gavana wa Nandi, Stephen Sang.
Kamati ya Fedha itaongozwa na Fernandes Baraza (Kakamega), Kamati ya Afya Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Kamati ya Kilimo na Ufugaji, Kenneth Lusaka (Bungoma), Mazingira, Wilber Otichillo (Vihiga), Maeneo Kame, Nathif Adam (Garissa), Uchumi wa Majini, Paul Otuoma (Busia), Elimu, Edwin Mutai (Kericho), Jinsia, Simon Kachapin (Pokot Magharibi), Ukusanyaji wa Raslimali na Ushirikiano, Simba Arati (Kisii), Masuala ya Sheria , Achillo Ayako (Migori).
Gavana wa Kisumu, Peter Anyang’ Nyong’o ataongoza Kamati ya Ardhi na Makazi, Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) itaongozwa na Wesley Rotich (Elgeyo Marakwet), Usalama na Masuala ya Kigeni Benjamin Cheboi (Baringo), Utalii Patrick Ole Ntutu (Kajiado), Usafiri na Kawi, Mohamed Ali (Marsabit), Maji Joshua Irungu (Laikipia) naye Sakaja akichaguliwa kuongoza Kamati ya Leba.
Akitoa hotuba yake ya mwisho kuhusu hali ya ugatuzi, Bi Waiguru alisema kaunti zimepiga hatua muhimu katika sekta kadhaa ikiwemo afya, elimu, utalii, na kawi, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo, Hazina Kuu haikusambaza kiasi chote cha Sh385.4 bilioni kilichotarajiwa kwa mgao wa bajeti ya 2023/2024, lakini badala yake ilisambaza Sh354.6 bilioni zilizopungua kwa asilimia nane.
Kiasi cha Sh46.36 bilioni kilichoorodheshwa kama mgao wa ziada kutoka kwa serikali kuu na washirika wa maendeleo hakikutimizwa huku kaunti zikipokea Sh29.07 bilioni tu.
Malimbikizi ya madeni yamesalia kero kuu kwa kaunti huku Sh182 bilioni zikiwa bado zinasubiri kulipwa.