Habari MsetoSiasa

Waiguru atarajia maseneta ‘kumtendea haki’

June 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na GEORGE MUNENE

HATIMAYE Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru amezungumzia masaibu yanayomkabili akielezea matumaini kwamba maseneta watazingatia kweli, haki na sheria watakapoanza kuchunguza hoja ya kumtimua afisini.

Bi Waiguru alisema hayo huku vijikaratasi vyenye maandishi ya kuwahimiza wakazi kufanya maandamano dhidi yake jana asubuhi vikisambazwa katika miji kadha ya kaunti ya Kiranyaga.

Kwenye taarifa fupi, kupitia akaunti yake ya twitter, dakika chache baada ya mawakili wake kuwasilisha stakabadhi zenye majibu yake kwa seneti Jumamosi jioni, Bi Waiguru alisema yu tayari kujitetea mbele ya kamati ya seneti Jumatano.

“Kama hatua ya kutimiza ombi la Seneti leo nimewasilisha majibu yangu kwa hoja iliyopitisha na Bunge la Kaunti ya Kirinyaga kuniondoa afisini. Naamini ukweli, haki na utawala wa sheria utadumishwa,” Bi Waiguru akasema.

Vijikaratasi vilivyoandikwa maneno “Waiguru Must go” (sharti Waiguru aondoke) vilisambazwa katika miji ya Kerugoya, Kimbimbi, Kianyaga, Kutus, Ngurubani an Kagio.

“Tuliamka asubuhi na kupata vijikaratasi vimetapakaa sehemu mbalimbali mjini,” mkazi mmoja wa Kimbimbi aliambia Taifa Leo.

Waandishi na wasambazaji wa vijikaratasi hivyo kuanzia Jumamosi usiku hawakujulikana.

Hiyo ndio ilikuwa taarifa ya kwanza, Gavana Waiguru kutoa tangu madiwani 23 kati ya 33 wa kaunti ya Kirinyaga walipopitisha hoja hiyo mnamo Juni 9, 2020; kwa tuhuma za kukiuka Katiba na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake.

Jumamosi jioni mawakili wa Waiguru, wakiongozwa na Kamotho Waiganjo, waliwasilisha katoni 40 zilizojaa stakabadhi kwa afisi ya karani wa Seneti, Jeremiah Nyengenye.

“Tumewasilisha majibu yote kwa tuhuma zilizoelekezewa gavana,” Bw Waiganjo ambaye pia ni mumewe Waiguru, aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

“Tumewasilisha stakabadhi zenye majibu yote. Gavana atafiki mbele ya Kamati ya Seneti juma lijalo kufafanua yaliyomo kwenye stakabadhi hizo,” akaongeza Bw Waiganjo.

Kamati hiyo maalum ya wanachama 11 na inayoongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ilibuniwa kuendesha uchunguzi kwa lengo la kubaini ikiwa mashtaka dhidi ya gavana huyo yana mashiko au la.

Kamati hiyo imemualika Spika wa Bunge la Kirinyaga Anthony Gathumbi kufika mbele yake mnamo Jumanne, Juni 23, kufafanua madai yaliyopelekea kupitishwa kwa hoja ya kutimua Gavana Waiguru.

Katika barua iliyoandikwa Juni 17 kwa Bw Gathumbi, kamati hiyo ilimshauri Spika huyo kuandamana na angalau madiwani watatu katika kikao hicho.

Aidha, kamati hiyo ilimtaka Spika huyo kutoa angalau nakala 200 za stakabadhi zote ambazo bunge hilo litatumia kuthibitisha makosa ambayo lilidai Waiguru alitenda.

Isitoshe, Bunge hilo lInahitajika kuwasilisha majina ya watu ambao watatoa ushahidi zaidi kuhusu suala hilo mbele yake.

Naye Bi Waiguru na kundi la mawakili wake wamealikwa kufika mbele ya Bw Malala, na wenzake, mnamo Jumatano, Juni 13, kujitetea.

Wameonywa kwamba endapo watakosa kufika, kamati hiyo itaendelea na shughuli zake na hatimaye kutoa uamuzi bila kushirikisha utetezi wao.