Waiguru 'hajapona'
Na CHARLES WASONGA
INGAWA Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ameipongeza Seneti kwa kutupilia mbali hoja ya kumwondoa afisini, hayuko salama kwani atachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Meneja wa tume hiyo ukanda wa Kati Charles Rasungu anasema wapelelezi tayari wametumwa katika serikali ya Kaunti ya Kirinyaga kuanzisha uchunguzi dhidi ya Waiguru.
Alisema afisi yake ilipokea malalamishi dhidi ya gavana huyo kuhusiana na madai kuwa aliingilia utoaji zabuni moja ya thamani ya Sh50 milioni na madai ya kupokea marupurupu kwa safari ya ng’ambo ambayo hakwenda.
Zabuni hiyo ilipewa kampuni ya Velocity Ltd ambayo inadaiwa kuwa haikutimiza vigezo vya kisheria kupewa zabuni hiyo.
“Malalamishi dhidi ya Gavana Waiguru yaliwasilishwa na raia wa kawaida katika afisi zetu mjini Nyeri mnamo Mei 30, 2020, na wala sio madiwani wa Kaunti ya Kirinyaga,” Bw Rusungu akasema.
Alisema maafisa wa EACC watachambua stakabadhi husika katika idara ya ununuzi ili kubaini ukweli kuhusu madai ya ukiukaji wa sheria katika utoaji zabuni.
Katika ripoti yake, kamati ya Seneti ilipendekeza kusimamishwa kazi kwa wanachama wote wa kamati ya zabuni kutoa nafasi kwa uchunguzi dhidi yao.
“Wale watakaopatikana na hatia waadhibiwe kama watu binafsi,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta wa Kakamega Cleophas Malala.
Mkurugenzi wa usimamizi
Miongoni mwa wale ambao maseneta walipendekeza wachunguzwe ni mkurugenzi wa usimamizi katika Kaunti ya Kirinyaga Pauline Kamau ambaye ilibainika kuwa ndiye aliyedaiwa kuendesha njama chafu kwa niaba ya gavana.
Wengine ni Bw Gichira Wayne ambaye ni mshauri wa gavana na mkurugenzi wa idara ya ununuzi Carilus Otieno aliyekuwa shahidi wa upande wa Waiguru.
Hata hivyo, Bw Malala alisema kuwa kamati yake haikupata ushahidi wa kumhusisha Gavana Waiguru, moja kwa moja, na sakata hiyo katika idara ya ununuzi.
“Hata hivyo, tumegundua kuwa baadhi ya zabuni zilikuwa zikipewa kampuni ambazo zina uhusiano na watu wanaoshikilia vyeo katika serikali ya Kaunti ya Kirinyaga,” akasema.
Lakini kamati hiyo ilimpata Bi Waiguru na hatia ya kupokea fedha kama marupurupu ya usafiri bila kusafiri, lakini ikasema “kosa kama hilo haliwezi kutumiwa kama msingi wa kumwondoa gavana afisini.”
“Hii ni hitilafu ya kiusimamizi ambayo inaweza kusuluhishwa kindani na maafisa wanaosimamia idara ya fedha,” akasema Bw Malala.
Lakini Bw Rusungu anasema suala hili, la kupokea malipo, ni miongoni mwa madai dhidi ya Gavana Waiguru ambayo yanachunguzwa na maafisa wa EACC.