Waititu, mkewe na mwanakandarasi kujua hatma yao Oktoba 2024 kuhusu kesi ya ufisadi
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu maarufu kama Baba Yao, mkewe Susan Wangari na mwanakandarasi walijitetea Jumanne Agosti 27, 2024 katika kashfa ya Sh588 milioni ya ujenzi wa barabara 2018 huku mahakama ikifunga kesi hiyo waliyoshtakiwa miaka mitano iliyopita.
Hata hivyo, Waititu alijipata taabani alipoulizwa jinsi alivyomuuzia mwanakandarasi Charles Chege shamba alilolipwa pesa zinazodaiwa zilitoka Kaunti ya Kiambu kabla ya kuwa mmiliki wake rasmi.
Kutokana na kuuziwa huko kwa shamba, hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani, Thomas Nzioki, alifahamishwa kwamba Bw Waititu alipokea kwa njia ya ufisadi zaidi ya Sh25 milioni kutoka kwa Bw Chege akijua pesa hizo zilipatikana kwa njia isiyo halali kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Kiambu, ambapo Waititu Gavana alikuwa.
Waititu alihudumu kama Gavana wa Kiambu kati ya 2017 na 2020.
Bw Chege ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya Testimonies Enterprises Limited (TEL) iliyoteuliwa kwa njia tata kujenga barabara katika Kaunti ya Kiambu, aliuziwa shamba lililoko Nairobi na Waititu.
Akijitetea, Bw Waititu alisema alipewa idhini ya kuuza shamba hilo mnamo Januari 2018, lakini hati alizotoa kortini kama ushahidi zilionyesha aliliuza bila hatimiliki.
Waititu, Susan na Charles Chege mmiliki wa TEL walijitetea na kuhojiwa na kiongozi wa mashtaka Faitha Mwila.
Waititu na wenzake walijaribu kujiondolea lawama katika kashfa hiyo.
Mahakama ilifunga kesi dhidi yake (kukamilika kuskizwa) na kuamuru itajwe Oktoba 3, 2024 washtakiwa wawasilishe ushahidi wao wa mwisho kabla ya hukumu kutolewa.
Waititu, mkewe na Chege wamekanusha mashtaka dhidi yao.
Wako nje kwa kwa dhamana.