• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Wakatoliki wasafiri Uganda kuwakumbuka wenzao 22 waliouawa

Wakatoliki wasafiri Uganda kuwakumbuka wenzao 22 waliouawa

NA RICHARD MAOSI

WAUMINI wa dhehebu la kanisa Katoliki kutoka Kenya wamefikisha siku 20 tangu waanze rasmi safari ya miguu kutoka Shamata, Nyahururu, wakielekea Namugongo, Uganda.

Safari hiyo iliyoanza Mei 7, inatarajiwa kutamatika Juni 6 takriban mwezi mmoja tangu wapige hatua yao ya kwanza.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, msemaji wao Fredrick Waweru, wazee, kina mama na vijana hufunga safari hiyo ya imani kila mwaka ili kuwakumbuka Wakristo 45 waliouawa na Mfalme Kabaka Mwanga II wa Uganda, kwa sababu ya msimamo wao thabiti katika imani ya Kikristo.

Wakristo hao walikuwa 23 wa Kianglikana na 22 wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamehubiriwa neno la Mungu na kugeuzwa Wakristo katika Ufalme wa Baganda. Waliuawa kati ya Januari 31, 1885 na Januari 27,1887.

Amri kutoka kwa Kabaka Mwanga ilitosha wao kukatwa vichwa na miili yao kuchomwa, ndipo kanisa la Katoliki likaweka hili katika kumbukumbu zao mnamo 1964 kuwakumbuka kwa maombi.

Waweru anasema waumini hutumia fursa hiyo kujitakasa, mbali na kuombea nchi inapokabiliana na jinamizi la ufisadi, mauaji ya kiholela,b aa la njaa na mashambulizi ya kigaidi.

Waumini wa dhehebu la katoliki wakisafiri kwa miguu kutoka Nyahururu kuelekea Namugongo Uganga kuadhimisha siku ya Wakristo waliouawa. Picha/Richard Maosi

“Kwa sababu ni safari ya hiari, washiriki wanahimizwa kuwa na uvumilivu kama Masihi Yesu alipokuwa ulimwenguni,” Waweru akasema.

Wakiwa chini ya Dayosisi ya Nyahururu wanatumia jukwaa hili kuikumbuka nchi hasa wakati huu wa misukosuko ya kisiasa.

Waumini wamekuwa wakisitisha safari katika sehemu mbalimbali za ibada na kupiga dua kabla ya kuendelea na mwendo .

Kasisi wa Dayosisi ya Nyahururu Joseph Mbatia amewarai wakristo kufuata kumbukumbu hizi kama njia mojawapo ya kumkaribia Mungu.

Pia amekuwa akiwahimiza vijana kufuata nyayo za watawa waliowawa nchni Uganda baina ya 1885-1887 wakitetea imani yao.

Caleb Ombongi ni mzee wa miaka 62,aliamua kujiunga na wakristo wenzake kutembea hadi Kampala Uganda kama washiriki wenzake.

Anasema hii ni mara yake ya pili kushiriki kwenye zoezi hili la kutembea maili nyingi hadi nje ya nchi yake.

“Mara ya kwanza nilitembea mnamo 2015,ninajaribu kila niwezalo kujilinganisha na watawa wa imani kwa kuyaombea matatizo ambayo yamekuwa yakinikabili kibinafsi,” aliongezea.

Kufikia Mei 30 inatarajiwa kuwa zaidi ya wakristo 80,000 watawasili Kampala Uganda pamoja na viongozi wao kutoka kila pande ulimwenguni.

 

 

You can share this post!

Shujaa hatarini kutemwa Raga ya Dunia

HYRAX HILL: Makavazi ya kipekee Nakuru

adminleo