Habari Mseto

Wakazi Lamu sasa watisha kuandamana kuhusu bandari

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu na viongozi wao wametoa makataa ya siku saba kwa serikali kutatua mizozo yote kuhusu mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET).

Pia wanataka kuwa na kikao na Rais Uhuru Kenyatta.

Wakazi hao wametoa makataa hayo huku wakitishia kufanya maandamano ya kila siku sawa na yale ambayo yamekuwa yakishuhudiwa jijini Mombasa kuhusiana na reli ya kisasa (SGR).

Kiegesho cha kwanza cha mizigo kwenye mradi wa LAPSSET eneo la Kililana, Kaunti ya Lamu kimepangwa kuzinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Novemba 8.

Wakazi hao walieleza hayo walipofika kwenye afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia ili kumkabidhi rasmi malalamishi yao.

Wakiongozwa na Mbunge wa Lamu Mashariki, Bw Athman Sharif, madiwani pamoja na wanachama wa mashirika ya kijamii, walimtaka kamishna kumfahamisha Rais kwamba jamii ya Lamu na viongozi wangetaka kukutana naye kwanza kabla ya uzinduzi wa kiegesho hicho.

Miongoni mwa malalamishi ambayo wanataka serikali kutatua kikamilifu ni suala la uteuzi wa wanachama wa bodi ya LAPSSET wanaodai ulibagua wakazi wa Lamu, ambapo hakuna hata mmoja ambaye aliteuliwa kuwakilisha jamii kwenye bodi hiyo.

Pia wanateta kuhusiana na ahadi ya serikali ya kufadhili vijana 1,000 wa Lamu ili kusomea kozi zitakazowawezesha kuajiriwa katika LAPSSET. Walisema kuwa kufikia sasa ni vijana 400 pekee ambao wamefadhiliwa kwa masomo hayo.

Vile vile, wanataka angalau asilimia 20 ya mapato kutoka kwa LAPSSET itengwe na kubaki Lamu ili kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kaunti ya Lamu na pia jamii ifaidike moja kwa moja na angalau asilimia tano

Pia waliitaka serikali kuhakikisha waathiriwa wote wa ardhi ya ekari 70,000 zilizotwaliwa ili kufanikisha mradi huo eneo la Kililana na Mashunduani , wanafidiwa kikamilifu.

Wakati huo huo, pia wanataka wavuvi wote zaidi ya 4,000 walioathiriwa na shughuli za mradi huo kufidiwa kwanza kabla ya ufunguzi wa kiegesho hicho.

Kutoridhishwa

Bw Sharif alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi serikali inavyoendelea kuibagua jamii ya Lamu kuhusiana na maamuzi yanayoambatana na mradi wa LAPSSET.

“Ikiwa mwito wetu utapuuzwa tena kufikia kipindi cha juma moja lijalo, basi serikali ijue dhahiri kwamba jamii ya Lamu haitarudi nyuma kamwe. Tutashiriki maandamano makubwa ya kila siku kama yale ya SGR mjini Mombasa hadi pale serikali itakaposikia kilio chetu,” akasema Bw Sharif.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Lamu ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Kiunga, Bw Abdalla Baabad, alisema haridhishwi na dhuluma ambazo serikali ya kitaifa imekuwa ikiendeleza dhidi ya jamii ya Lamu.

“Kaunti ya Turkana ambako serikali inaendeleza mradi wa uchimbaji mafuta tayari wamehakikishiwa asilimia 20 ya kodi ya mapato kwa serikali ya kaunti ili kutekelezea miradi ya maendeleo. Asilimia nyingine tano pia inaendea jamii ili kuinufaisha moja kwa moja. Kwa nini sisi wakazi wa Lamu ambao tuko na mradi wa kimataifa wa LAPSSET tunabaguliwa kihaki?” aliuliza.

Aliongeza, “Wajue kwamba licha ya mradi wa LAPSSET kuwa wa kimataifa, uko Lamu na lazima jamii itambuliwe na inufaike. Hilo hatuombi bali tunataka.”