Wakazi mijini wanavyofurika sokoni kununua bidhaa za kula kukwepa makali ya maandamano
WAKENYA wamebuni mikakati mipya kujipanga kimaisha wakati huu kunaposhuhudiwa maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha Mwaka 2024.
Uchunguzi wa Taifa Dijitali unaonesha kwamba wakazi jijini Nairobi hufurika masokoni na madukani kununua bidhaa kabla ya siku iliyopangiwa kufanyika maandamano.
Mwanyekiti wa Soko la Muthurwa, Nelson Githaiga Waithaga alikiri kwamba wafanyabiashara wamekadiria hasara kubwa kufuatia maandamano ya vijana akisema wafanyabiashara hufunga biashara wakihofia mali yao kuharibiwa.
Hata hivyo, alibaini kwamba wafanyabiashara hupata faida kuuzia wateja bidhaa siku moja kabla ya maadamano kufanyika kwa nia ya kujiwekea akiba kwani haitabiriki ikiwa ghasia na fuzo zitaendelea baada ya siku iliyoratibiwa kufanyika.
“Wafanyabiashara huuza sana tukikaribia siku ya maandamano, watu wakijiwekea akiba ya bidhaa hasa vyakula kutoka soko letu wakihofia hatutafungua biashara,” Bw Githaiga akasema.
Alilalamikia huduma zao kuathirika pakubwa, bidhaa zisizohifadhika kwa muda mrefu zikioza ikizingatiwa wafanyabiashara wengi hawana miundomsingi bora.
Isitoshe, shughuli za usafirishaji mazao kutoka shambani Githaiga anasema hutatizika kwa sababu wenye magari huhofia yasivamiwe na waandamanaji.
“Kukiwa na machafuko, hakuna mtu atathubuti kupeleka gari lake barabarani akihofia lisiteketezwe. Hali hiyo huchangia bidhaa kuharibikia mashambani,” akaongeza.
Gen Z wameapa kuendeleza maandamano hadi pale serikali ya Rais William Ruto itaangazia matakwa yao, ikiwemo gharama ya maisha kupanda na kukosa ajira.