• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wakazi wa Juja wanaopitia hali ngumu waisihi serikali iwapelekee chakula

Wakazi wa Juja wanaopitia hali ngumu waisihi serikali iwapelekee chakula

Na LAWRENCE ONGARO

WAKFU wa Jungle Foundation unazuru maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Kiambu kwa minajili ya kutoa chakula na vifaa vya kujikinga dhidi ya Covid-19.

Siku chache zilizopita wakfu huo ulizuru vijiji vya Gatuanyaga na Ngoliba, Thika Mashariki, ambapo walisambaza chakula, barakoa, sabuni na kuwahamasisha wakazi wa maeneo hayo.

Afisa anayesimamia mpango huo Bw Eliud Macharia, amesema kulingana na uchunguzi wao, wakazi wa mashinani wanapitia masaibu mengi kwa sababu hawana njia yoyote ya kujikimu.

“Wakati huu wananchi wanapokabiliana na Covid-19, mambo yamekuwa magumu ajabu kwa sababu watu wengi wanakaa hata siku mbili bila kupata cha kutia tumboni,” akasema Bw Macharia.

Mkurugenzi mkuu wa wakfu huo wa Jungle Foundation, Bw Patrick Wainaina ambaye ni mbunge wa Thika, amesema wananchi wengi wanastahili kuhamasishwa pakubwa kuhusu Covid-19.

“Maafisa wangu wamezuru mahali kwingi na kupata ya kwamba wengi hawazingatii maagizo yaliyowekwa kama kuvalia barakoa na kuweka nafasi ya mita moja au zaidi baina ya mmoja na mwingine,” akasema Bw Wainaina.

Amesema hiyo ndiyo maana aliamua kuzunguka Kaunti ya Kiambu ili kuwajali wananchi wanaostahili msaada.

Na Ijumaa, zaidi ya barakoa 500 na mitungi 20 ya maji ya kunawa mikono imetolewa kwa wakazi wa kijiji cha Gachororo, Juja, kupitia wakfu huo.

Afisa wa afya wa Wakfu wa Jungle Foundation Afya, ampima halijoto mkazi mmoja wa Juja, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Lawrence Ongaro

Mkazi wa Gachororo Bw Hassan Busolo amesema corona imesababisha masaibu kwa watu wengi.

“Mimi nilifutwa kazi miezi miwili iliyopita na wakati mwingine namaliza hata siku mbili bila kupata chakula. Serikali ijaribu ituletee chakula,” akasema Bw Busolo.

Naye mkazi mwingine Bi Nelly Akoth ambaye ni mama ya watoto watano anasema biashara yake ya samaki iliharibika kwa sababu wateja wamepungua. Hata wamekosa maji eneo hilo na kwa hivyo lazima wazingatie afya ya wananchi.

Naye mkazi wa Juja Bw Linus Munyonge amesema vijana wengi wamekosa kazi maalum ya kufanya baada ya viwanda vingi eneo hilo kufungwa.

Anasema ufukara umezonga wakazi wa eneo hilo ambapo hata kupata pesa za kununua chakula imekuwa ndoto kwao.

“Tunataka serikali ifanye hima isambaze chakula eneo hili lakini hatutaki mapendeleo kama inavyoshuhudiwa kila mara chakula hicho kikiletwa,” akasema Bw Munyonge.

Naye Bw John Mwaura ambaye ni kijana wa eneo hilo anasema vijana wengi wameachwa bila chochote huku wakibaki kuketi bure.

“Sisi tunataka serikali pia ituajiri kama wale wanaoajiriwa kwingineko kama sehemu ya kutii amri ya Rais Uhuru Kenyatta ya hivi majuzi,” akasema Bw Mwaura na kuongeza vijana wengi wana familia changa na hawana mtu yeyote wa kulilia.

You can share this post!

Wasio na uwezo kusikia kutumia maski spesheli kusoma midomo...

MWANAMKE MWELEDI: Alipambana kuhakikisha wakulima wadogo...

adminleo