Wakazi wa Likoni wapewe ajira Dongo Kundu – Mishi Mboko
Na SAMUEL BAYA
MBUNGE wa Likoni, Bi Mishi Mboko Jumanne alisema wakazi wa Mtongwe, Mwangala na Mbuta wanafaa kuajiriwa katika mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa katika eneo la Dongo Kundu.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Mboko alisema kuwa licha ya mradi huo kuwa muhimu kwa taifa la Kenya, wao kama wakazi sharti wapatiwe nafasi ya kwanza katika ajira.
“Mimi nimeongea na mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya bandari nchini(KPA), Dkt Daniel Manduku na kumtaka awape ajira wakazi wa Likoni.
Kwa miaka mingi, kumekuwa na dhana kwamba wakazi wa Likoni bado hawajasoma lakini hali kwa sasa ni tofauti,” akasema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema kuwa kuna takribani nafasi 55,000 za kazi ambazo zitaletwa na mradi huo na wakazi lazima wawe watu wa kwanza kupata ajira.
“Sisi tuko na vijana wetu ambao wanaweza kufanya kazi hizi zote, kuanzia zile za mikono, au hata zile za afisini. Likoni hii imejaa wahandisi na KPA lazima ifahamu hilo, vijana wetu wamesoma na shahada tele zimejaa afisini kwangu,” akasema mbunge huyo.
Alitishia kufanya maandamano na wakazi hadi katika afisi kuu za halmashauri hiyo endapo wakazi wake hawatapatiwa nafasi za kazi.
“Mimi nikiwa nimefanya juhudi zangu zote mpaka nimemaliza na imeshindikana, sitakuwa na la ziada ila kuchukua wakazi hadi katika afisi za KPA na kuandamana hapo.
Hatuwezi kuwa na bandari hii hapa kisha wananchi wanaendelea kupata shida kila wakati, lazima nasi tufaidike,” akasema Bi Mboko.
Mbunge huyo alisema kuwa licha ya katiba kueleza kwamba jamii ambazo zinaishi katika maeneo kuliko miradi fulani lazima zifaidike, halmashauri hiyo bado inayumba katika kuajiri wakazi wa Likoni.
“Katiba iko wazi kwamba kila kunapofanyika mradi, lazima wakazi wa pale wawe watafaidika. Lakini ni masikitiko makubwa sana kwamba bandari imekuwa kwetu kama watu wa Likoni, wafanyakazi ambao wanatoka eneo bunge la Likoni ni wachache sana,” akasema.
“Sio kwamba watoto wetu hawatumi maombi, wanatuma sana. Hivi majuzi kulikuwa na matangazo ya kazi katika mtandao na vijana wengi walituma maombi.”
Aliongeza, “Mimi binafsi nilisaidia katika kusambaza ujumbe lakini pia hawakufaulu. Kama washikadau wakubwa sisi kama watu wa Likoni, tunasikitika kwamba hawajapata kazi.”
Mbunge huyo alisisitiza kuwa wakazi hao wanafaa kuzingatiwa kwanza katika ajira yoyote.
“Sasa kama wananchi wetu hawatapatiwa ajira hasa katika mradi huu mkubwa unaokuja, basi nitawachukua mpaka bandarini kuandamana. Sisi kama wakazi wa Mombasa, tunasema kuwa bandari ya Mombasa ndio shamba letu ambalo tuko nalo na vijana wetu lazima wanufaike pia,” akasema mbunge huyo.
Alhamisi iliyopita, mbunge huyo alikuwa miongoni mwa wakazi ambao walihuhudhuria mkutano wa uhamasisho kuhusiana na mradi wa ujenzi wa eneo la biashara la kisasa katika bandari ya Dongo Kundu pamoja na ujenzi wa barabara ya kisasa.
Mradi huo unatarajiwa kutumia zaidi ya Sh30 billioni za serikali.