• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Wakazi wa mtaa wa Landless walalama kuhusu ongezeko la visa vya wizi

Wakazi wa mtaa wa Landless walalama kuhusu ongezeko la visa vya wizi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa mtaa wa Landless mjini Thika wanaitaka serikali iimarishe usalama wakisema wezi wamezidi.

Wanasema wezi hao huvamia makazi yao usiku wa manane wakiwa wamejihami kwa silaha hatari.

Maeneo yanayolengwa sana ni Barabara ya Cairo, na Riverside ambako wanapulizia watu dawa za usingizi.

“Mimi nilipata fahamu mwendo wa saa mbili za asubuhi ambapo nilipata vyombo vya kutoka kwa nyumba yangu vikiwa vimeibwa. Kumbe walikuwa wamevunja mlango wa nyuma walikoingilia,” alisema mkazi wa Landless Bw Martin Kamau.

Anasema mnamo Jumatatu asubuhi alipata runinga yake imeibwa, pasi ya stima, mtungi wa gesi ya kupikia, na pia sufuria.

Wakazi hao wanasema hali hiyo imewatia wasiwasi ambapo wanataka walinda usalama waingilie kati na kuwatia nguvuni wezi hao.

Inadaiwa pia wezi hao wanatembea kwa kikundi kikubwa wakiwa wamejihami kwa vifaa kama panga, shoka, na hata nyundo.

Naye Bi Jane Wanjiru, alisema aligundua wezi hao waliiba kila kitu kilichokuwa jikoni.

“Maziwa yaliyokuwa ndani ya friji, na matunda yaliibwa na wezi hao. Hata nashangaa ni vipi waliingia chumbani kwangu bila mimi kusikia,” alisema Bi Wanjiru.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Thika, Bi Beatrice Kiraguri, amesema amepata habari hizo na tayari uchunguzi unaendelea.

“Tayari tumeanza uchunguzi ambapo maafisa wa polisi watashika doria katika eneo hilo,” alisema afisa huyo.

Amesema tayari wakazi wachache wameandikisha taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Tayari wakazi hao wamefanya mkutano wa dharura ili kujadiliana kuhusu matukio hayo na jinsi wanavyostahili kujilinda.

Wamesema watatilia zingatio mpango wa Nyumba Kumi ili kufanikisha juhudi zao za kupambana na uhalifu katika mtaa wao.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunaungana kwa pamoja kuona ya kwamba hali ya usalama katika eneo letu inapewa kipaumbele,” akasema Peter Karanja ambaye ni mkazi wa mtaa huo.

You can share this post!

Moi alipotoweka kwa wiki moja…

Wanaume wako katika uwezekano mkubwa kupata maambukizi ya...

adminleo