• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Wakazi wa Munyu wanufaika na mradi wa maji

Wakazi wa Munyu wanufaika na mradi wa maji

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Munyu, Kaunti ya Kiambu, watanufaika pakubwa na mradi wa maji uliozinduliwa Jumanne chini ya ufadhili wa Jungle Foundation.

Wakazi hao wamekuwa wakiteta kwamba kwa muda wa miaka 40 wamekuwa wakitumia maji ya Mto Athi ambao umekuwa ukiingizwa kila aina ya majitaka kutoka viwanda vya karibu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliingilia kati baada ya wakazi hao kudai kuwa wakazi, hasa wanawake wengi wamekuwa wakisafiri mwendo mrefu kutafuta maji hayo ya mto huku wakipanda milima na mabonde.

“Baada ya kupata malalamishi mengi ya wakazi wa Munyu, nililazimika kuzindua mradi wa ‘Munyu Community Water Project’ ambao umekamilika kwa sasa na utawafaa wakazi wapatao 20,000 ndani na nje ya eneo hili,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza vijana kujiunga kwa vikundi ili kuanzisha mpango wa kilimo akisema yuko tayari kuwapa msaada.

“Iwapo vijana watakubali kuungana pamoja kwa lengo moja la kuboresha kilimo, bila shaka niko tayari kuwapiga jeki,” alisema Bw Wainaina.

Alisema cha muhimu ni kwamba shule mbili muhimu; Munyu Secondary na Munyu Primary, zitanufaika pakubwa kwa sababu hakuna shida ya kwenda kutafuta maji tena.

“Hata kilimo kitaimarika pakubwa kwa sababu mboga za spinachi, maharage, na kabeji zitanawiri kwa wingi katika eneo hili,” alisema Bw Wainaina.

Kuzinduka

Alisema mradi huo umegharimu takribani Sh3 milioni na ana matumaini wakazi wa eneo hilo watazinduka na kuzingatia kilimo zaidi.

“Sisi kama wakazi wa hapa tunashukuru kupata maji hapa karibu na makazi yetu. Sasa shida ya kutembea mwendo mrefu imekwisha kabisa.Tutazidi kuendesha kilimo kwa fujo,” alisema Bi Jane Wangari Kimani ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Bw Wainaina aliwashauri vijana kujiepusha na pombe aina ya chang’aa na bangi ambayo inadaiwa kuwateka nyara vijana wengi katika eneo hilo.

“Ninahimiza maafisa wa usalama na wazazi wapambane na jambo hilo haraka iwezekanavyo kwa sababu tukiachilia hivyo, vijana hawa wataangamia kimaisha,” alisema Bw Wainaina.

You can share this post!

Nia yetu si kumng’oa Uhuru madarakani –...

Victor Wanyama apata jeraha la goti

adminleo